1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Samia asema yuko tayari kuvumilia na kusamehe

Deo Kaji Makomba
15 Desemba 2021

Rais Samia Suluhu,amesema yuko tayari kusikiliza,kuvumilia na kusamehe yote yanayoelekezwa kwake na upinzani, ingawa anataka pia kuona vyama hivyo vikifanya kazi zake kwa kuzingatia sheria.

Tansania Präsidentin  Samia Suluhu Hassan
Picha: Eric Boniphase/DW

Akizungumza kwenye mkutano huo wa kwanza kwake kukutana moja kwa moja na vyama vya siasa, Rais Samia aliyeingia madarakani miezi saba iliyopita kufuatia kifo cha mtangulizi wake, John Magufuli, aliyepiga marufuku mikutano ya hadhara, amewaambia washiriki kwamba atambuwa kuwa ni haki yao kukusanyika na kutangaza sera zao, na kuutaka mkutano huo kuja na mapendekezo ya kuhakikisha kuwa hilo linafanyika kwa kuzingatia sheria na taratibu za nchi.

''Ni vyema vyama vya siasa mnapofanya shughuli zenu mzingatie hayo na kwamba kuwa na mfumo wa vyama vingi na mawazo mbadala haimanishi kuwepo vurugu, fujo kali zenye ukakasi,vitisho na zenye kuamsha hisia za kuleta vurugu na uvunjifu wa amani.'',alisema Samia.

Kusamehe na kuzika tofauti

Katika mkutano wa wadau na viongozi wa vyama vya siasa unaolenga kujadili hali ya demokrasia ya vyama vingi vya siasa nchini Tanzania, Rais Samia ametaka pawepo na utaratibu wa kujadiliana kwa busara, kuelekezana, na kuelimishana ili kuimarisha demokrasia ya nchi. Aidha amesema kuwa yupo tayari kusamehe na kuzika tofauti za nyuma zilizosababishwa na uchanga wa demokrasia.

Ama kuhusu asasi za kiraia Rais Samia amezitaka kuiga mfano uliooneshwa na Baraza la vyama vya siasa kukutana na kujadiliana kwa lengo la kurekebishana ili kuondoa migongano kati ya serikali na wananchi.

''Tufanye siasa kwa tija kwa maslahi ya nchi''

Freeman Mbowe,kiongozi wa chama cha upinzani cha CHADEMAPicha: Ericky Boniphace/DW

Awali kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Zuberi Kabwe, akitoa salaam zake amesema kuwa Tanzania inakabiliwa na changamoto za kisiasa na kumuomba Rais Samia kuuwaunganisha Watanzania ambao wameparaganyika. Kadhalika amemuomba Rais kuangalia suala kiongozi wa chama kikuu cha upinzani, CHADEMA, Freeman Mbowe, ambaye kwa sasa anashikiliwa kwa tuhuma za ugaidi.

''Tunakuomba sana sana sana kwa mujibu wa sheria na kufata taratibu zote za kisheria, tusaidie mwenzetu ( Freeman Mbowe) tuwe naye ili tuweze kufanya kazi kwa pamoja,tuunganishe nchi yetu, tufanye siasa kwa tija kwa maslahi ya nchi.'',alisema Zitto.

Rais Samia amemaliza kufungua mkutano huo muda mfupi uliopita, mkutano ambao umewakutanisha wadau wa siasa wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa na asasi za Kiraia.