1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Samia amsimamisha kazi mkurugenzi mkuu wa bandari

Josephat Charo
28 Machi 2021

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amepokea ripoti ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali na taasisi ya kupambana na rushwa. Ameamuru Mkurugenzi wa mamlaka ya Bandari asimamishwe kazi.

Tansania Dodoma | Präsidentin Samia Suluhu Hassan
Picha: Habari Maalezo

Rais Samia ametoa maagizo hayo Jumapili (28.03.2021) ikulu jijini Dodoma, wakati akipokea ripoti kutoka kwa mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali nchini humo, CAG, Charles Kichele, pamoja na ile ya taasisi ya kupambana na rushwa TAKUKURU ya mwaka 2019 na 2020.

Rais Samia, katika maagizo yake, amemtaka Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali kwa kushirikiana na gavana wa benki kuu kufuatilia fedha zote zilizotoka kuanzia mwezi wa Januari hadi  Machi mwaka huu kwa ajili ya miradi ya maendeleo ili zionekane kama zimefanya kile kilichokusudiwa au la. 

Katika hotuba aliyoitoa wakati wa kupokea ripoti hizo mbili muhimu kutoka kwa CAG na TAKUKURU, Rais Samia amesema kuwa kuna ubadhirifu mkubwa wa mabilioni ya shilingi na kumtaka mkurugenzi wa TAKUKURU, Brigedia Jenerali John Mbungo, haraka kuimurika Mamlaka ya bandari huku mkurugenzi wa mamlaka hiyo, Deusdedit Kakoko, akisimamishwa kazi kupisha uchunguzi.

Ripoti ya CAG kulingana na Rais Samia inaonyesha kuna upotevu wa zaidi ya shilingi bilioni tatu katika Shirika la Bandari nchini humo. 

Mama Samia aimulika TAMISEMI

Katika hatua nyingine Rais Samia Suluhusu Hassan ameinyooshea kidole Wizara ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na serikali za Mitaa TAMISEMI iliyopo chini ya Waziri Selemani Jafo, kuwa kuna upotevu mkubwa wa fedha katika Wizara hiyo na kumtaka waziri huyo kusimamia mapato na matumizi ya wizara hiyo na akishindwa aseme ili asaidiwe. 

Rais Samia pia amegusia kuhusiana na suala la rushwa ya ngono katika vyuo vikuu nchini Tanzania na kusema kuwa utafiti wa rushwa ya ngono katika vyuo uangaliwe kwa kina, kama katika eneo la uvujishaji mitihani. Kadhalika Rais Samia ametoa maagizo mbalimbali ikiwemo ofisi ya mkaguzi mkuu wa serikali CAG ripoti yake kuwa wazi zaidi.

Taasisi ya kupambana na kuzuia rushwa Tanzania, TAKUKURU imetakiwa kushughulikia kwa haraka kesi zilizopo na zisirundikwe, kesi zisizo na mashiko zisipelekwe mahakamani, sheria za mashahidi ziangaliwe upya, kiwepo kipengele cha kulinda mashahidi, maana kumekuwa na taarifa za mashahidi kufahamika na hatimaye kuleta fitina kati ya shahidi na mshitakiwa. 

Pia ametaka kuimarisha mifumo ya mamlaka ya kupambana na rushwa, kudhibiti matumizi mabaya ya ofisi, kubuni na kutekeleza mikakati mipya ya kupambana na rushwa, kuharakisha na kuishirikisha jamii katika mapambano dhidi ya rushwa. Mama Samia aliongeza kuwa atasimama imara katika kupambana na rushwa.

Na Deo Kaji Makomba

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW