1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Samia Suluhu ateta na wakuu wapya wa mikoa

19 Mei 2021

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amefanya kikao cha ndani na wakuu wa mikoa wapya aliowaapisha katika kile kilichoelezwa ni kuwapa maelekezo ya kiutendaji wakati anapoendelea na hatua za kuisuka upya serikali yake.

Tansania l Neue Präsidentin Samia Suluhu Hassan
Picha: AP/picture alliance

Licha ya matarajio ya wengi kwamba Rais Samia angetumia jukwaa hilo la kuwaapisha watendaji kuzungumzia masuala mbalimbali, hata hivyo kiongozi huyo aliyekuwa ameambatana na watendaji wengi kadhaa alibadili mwelekeo kwa kufanya mazungumzo ya ndani na wateule wake hao.

Imefahamika kuwa, Rais Samia alikuwa na lengo la kuwapa maagizo yapi wanapaswa kuyazingatia wakati huu wanapoenda kuanza majukumu yao mapya na masuala yapi watapaswa kuyaepuka ili kuendelea kulinda imani ya wananchi juu ya utendaji wa serikali yake inayosisitiza umuhimu wa kutenda haki , kuepuka uenevu na kuweka dhamira ya kuwa karibu na wananchi.

Viongozi hao ambao sasa wanatarajiwa kuwasili katika vituo vyao vya kazi, wameaswa kutovimba mabega wakiwa kwenye maeoneo yao bali wanachopaswa kutambua kutambua ni kuwa nafasi walizopewa ni kwa ajili ya kuwatumikia wananchi kwa kutenda haki.

Spika wa bunge la Tanzania Job NdugaiPicha: DW/E. Boniphace

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Tanzania, Job Ndugai ni miongoni mwa viongozi waliotoa maeneo ya moja kwa moja kwa wateule hao akiwakumbusha tabia ya kujitwalia madaraka mikononi wawapa kwenye vituo vya kazi ni kwenda kinyume na sheria.

Katika utawala uliopita, wakuu wa mikoa pamoja na wilaya walitupiwa lawama mara kwa mara kutokana na mwenendo wao wa kuwa sehemu ya migogoro kama vile maamuzi yao ya kuwaweka mahabusu wananchi pindi inapotokea mvutano wa jambo fulani.

Tangu aiingie madarakani mwezi Aprili Rais Samia amekuwa akiisuka serikali yake kwa awamu na huenda sasa akawageukia wakuu wa wilaya na maafisa wengine, baada ya kufanya hivyo kwa mawaziri na baadhi ya vigogo wa mashirika ya umma.

Mwandishi: George Njogopa/DW Dar es Salaam

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW