Rais Samia ataja baraza la mawaziri, lina wizara mbili mpya
17 Novemba 2025
Rais Samia Suluhu Hassan ametangaza baraza jipya la Mawaziri, likiwa na wizara mpya mbili, Wizara ya kazi, Ajira na Mahusiano na Wizara ya Vijana.
Hatua ya kuundwa kwa wizara hizi imekuja ikiwa siku chache baada ya rais kulihutubia bunge Novemba 14 akitoa ahadi ya kuunda wizara kamili ya Vijana itakayosikiliza na kufanyia kazi changamoto za vijana ambayo itakuwa chini ya ofisi ya rais.
Akizungumza na wanahabari leo Ikulu ya Chamwino, Dodoma, Rais Samia amesema amefanya marekebisho kidogo wizara ya kazi na ajira na kuongeza kipengele cha mahusiano ambacho kitafanya kazi na makundi mbalimbali ili kujenga mahusiano mazuri.
Nani kaingia?
Waliochaguliwa kushika nafasi katika wizara hizo mpya ni Joel Arthur Nanauka, Waziri wa Maendeleo ya Vijana na Deus Clement Sangu, Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo.
Sura mpya zilizoingia kwenye baraza la mawaziri ni pamoja na Paul Christian Makonda aliyeteuliwa kuwa Naibu waziri wa Pili, Wizara ya habari Utamaduni, Sanaa na Michezo na Wanu Hafidh Ameir akichaguliwa kuwa Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia na Nanauka ambaye anaongoza Wizara ya Vijana.
Pamoja na sura hizo mpya, wapo mawaziri wa zamani ambao nafasi zao zimezibwa na mawaziri wengine, akiwamo aliyekuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Dotto Biteko; Hussein Bashe aliyekuwa (Kilimo); Innocent Bashungwa aliyekuwa (Mambo ya Ndani); Jenista Mhagama aliyekuwa (Afya); na Dkt. Seleman Jafo aliyekuwa (Viwanda na Biashara).
Kadhalika Rais Samia amewateua Balozi Khamis Musa Omar, kuwa waziri wa Fedha, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, Waziri wa Mambo ya nje na Ushirikiano wa kimataifa na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ikiongozwa na Angella Kairuki.