1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Samia: Tuweke mazingira mazuri kwa wawekezaji

Hawa Bihoga6 Aprili 2021

Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewataka watendaji wa serikali kuhakikisha wanaweka mazingira muafaka kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ili kustawisha uchumi wa nchi hiyo.

Tansania Dodoma | Präsidentin Samia Suluhu Hassan
Picha: Habari Maalezo

Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewataka watendaji wa serikali kuhakikisha wanaweka mazingira muafaka kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ili kustawisha uchumi wa nchi hiyo na kuacha urasimu na unyanyasaji dhidi ya kundi hilo muhimu kwa ustawi wa uchumi wa nchi.

Rais Samia amesema hayo baada ya kuwaapisha makatibu wakuu wa wizara mbalimbali na manaibu wao.

Soma zaidi: Rais Samia Suluhu amsimamisha kazi mkurugenzi wa mamlaka ya bandari

Licha ya Tanzania kutangazwa kuingia kwenye uchumi wa kati mwaka uliopita, Rais samia suluhu amesema, hali ya kiuchumi bado ni ngumu kutokana na wawekezaji wengi kuamua kuhamisha biashara zao katika mataifa mengine kufuatia kile alichokitaja kuwa ni urasimu na unyanyasaji wa baadhi ya watendaji serikalini.

Rais Samia ambae bado yupo kwenye mchakato wa kusuka upya safu yake ya uongozi, amekiri kuwa Tanzania inawahitaji zaidi wawekezaji kuliko wao wanavyohitaji kuwekaza katika nchi hii ambayo idadi yake ya watu inakaribia milioni 68.

Akitilia mkazo hoja yake ya kurahisisha mazingira ya uwekezaji Rais huyo wakwanza mwanamke wa Tanzania ameitaka ofisi ya waziri mkuu, kuhakikisha wanaondoa urasimu katika mchakato wa kutolewa kwa vibali vya kazi kwa wawekezaji na kuwataka kuacha mara moja kuwalazimisha wawekezaji kuajiri wafanyakazi wa kitanzania kwani wanao uhuru wa kuchagua wa kufanya nao kazi.

Rais Samia ataka watendaji kuhakikisha wanaondoa urasimu katika mchakato wa kutolewa kwa vibali vya kazi kwa wawekezaji

Mfanyabiashara katika soko la Kariakoo, mjini Dar es Salaam.Picha: DW/E. Boniphace

Rais suluhu pia amegusia uamuzi wake wa kumteua Balozi Lebarata Mulamula kushika uadhifa wa waziri wa mambo ya nje akisema kutokana na uzoefu wa mwanamama huyo, matarajio yake ni kuliona taifa likiboresha mahusiano yake na mataifa ya nje, kwani Tanzania si kisiwa inahitaji mashirikiano.

Kadhalika amewakumbusha watendaji wa wizara hiyo kuwa wao ni wawakilishi jamhuri ya muungano hivyo katika utendaji wao wanawajibika kuwakilisha maslahi ya pande mbili za muungano.

Wachambuzi na wakaazi waelezea matarajio yao katika utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan

02:38

This browser does not support the video element.

Katika kuendeleza kile ambacho kiliachwa na mtangulizi wake hayati dokta John Magufuli, Rais Samia amewataka watendaji katika wizara ya viwanda kuhakikisha wanatengeneza kanzi data ya viwanda vyote vinavyoendeleza shughuli zake hapa nchi kadhalika kuendeleza miradi yote ya maendeleo ilioachwa katika serikali iliopita.

Awali makamu wa Rais dokta Philip Mpango na waziri Mkuu Kassim Majaliwa, wamewataka watendaji wote wa serikali walioaminiwa na Rais kuhaklikisha wanaweka mipango madhubuti ya kufanikisha malengo ya serikali ya awamu ya sita, yenye kuhakikisha inafikisha faida za kiuchumi wa kati kwa mtu mmoja mmoja.

Baada ya kuwaapisha mawaziri, makatibu wakuu na manaibu wao pamoja na baadhi ya wakuu wa taasisi za serikali, Rais Suluhu ameweka wazi kuwa sasa atawatazama pia wakurugenzi wa halmashauri mbalimbali.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW