Rais Samia: Vyombo vya habari vinapaswa kufuata sheria
17 Februari 2022Kauli hiyo ameitoa katika mahojiano maalum aliyoyafanya na Idhaa ya Kiswahili ya DW mjini Brussels, Ubelgiji ambako anahudhuria mkutano wa kilele wa siku mbili kati ya viongozi wa Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya.
Katika mahojiano hayo aliyofanyiwa na Sudi Mnette kwa ushirikiano wa Mohammed Khelef, Rais Samia amesema serikali iko tayari kupokea mapendekezo kuhusu marekebisho ya sheria ya huduma za habari ya mwaka 2016, ambapo nyingine zimeelezwa kuwa kandamizi.
Mbali na kuzungumzia uhuru wa vyombo vya habari nchini Tanzania, Rais Samia amesema kuwa Tanzania ipo mbioni katika jitihada za kuanzisha kiwanda cha kutengeneza chanjo ya COVID-19 na nyinginezo kwa lengo la kunusuru afya ya umma wa taifa hilo pamoja na kuokoa fedha nyingi ambazo taifa hilo linazitumia katika kununua chanjo.
Aidha, Rais Samia amezungumzia pia masuala kadhaa ikiwemo matarajio yake kuhusu mkutano kati ya viongozi wa Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya, uhusiano kati ya Tanzania na Ulaya, kesi ya kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Freeman Mbowe pamoja na mazungumzo yake aliyoyafanya na makamu mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu anayeishi uhamishoni nchini Ubelgiji.
Kuhusu suala la kuyalinda mazingira, Rais Samia amezitaka nchi zenye uwezo mkubwa wa kiuchumi na hasa zenye kubeba lawama katika uchafuzi wa mazingira duniani zitekeleze ahadi zao kwa vitendo za michango ya fedha ili kudhibiti athari zinazoongezeka za mabadiliko ya tabianchi kwa mataifa ya Afrika, ikiwemo Tanzania.
Kwa mahojiano zaidi tembelea chaneli yetu ya Youtube ambako utaona pia vidio kuhusu mahojiano hayo. https://youtu.be/d_si_fpjZ5w