Rais Samia wa Tanzania akamilisha ziara ya Rwanda
3 Agosti 2021Kutembelea viwanda kulikuwa ni mwendelezo wa kukamilisha ratiba yake aliyoianza hiyo jana. Leo ilipangwa kwamba Rais Samia Suluhu Hassan angevitembelea viwanda hivi. Mapema alikitembelea kiwanda cha Inyange ambacho pamoja na mambo mengine, ndicho cha kwanza nchini kwa uchakachaji wa maziwa, juisi na vinywaji vingine laini.
Baadaye Rais Samia akiwa na mwenyeji wake Rais Paul Kagame wa Rwanda walitembelea kiwanda kingine cha Mara phones ambacho kazi yake ni kutengeneza simu za kisasa za mkononi maarufu kama smart phone.
Kiwandani hapo alishuhudia jinsi simu hizi zinavyotengeneza na kila hatua simu inakopitia hadi kuwa simu inayotumiwa kwa huduma.
Baadaye ya hapo alikitembelea kiwanda cha kampuni ya Kijerumani ya Volkswagen kinachounda magari yake nchini Rwanda.
Humo mote Rais Samia hakuweza kungumza na vyombo vya habari. Hata hivyo, nimezungumza na mmoja wa wamiliki wa viwanda kutoka Tanzania, Khardi Fessa, na akawa na haya ya kusema: Uhusiano huu ambao ni matokeo ya ujenzi wa viwanda vya Watanzania nchini Rwanda umewanufaisha pia wananchi wa Rwanda, hasa waliokwishapata ajira kwenye viwanda hivi:
Tunapenda tuone wawekezaji zaidi kutoka nchi za nje mathalan kutoka Tanzania kwa sababu Rwanda kuna wafanyakazi wazuri na wenye adabu, na kwa sababu hiyo tunaamini mwekezaji akija atapata faida bila tatizo
Haya ni matokeo ya kazi nzuri ya serikali chini ya uongozi wa Rais Paul Kagame ambayo inawaleta wawekezaji kuwekeza Rwanda na sisi tunapata kazi na fursa nyingine na sisi tuko tayari kuboresha kazi zaidi.
Ijapokuwa leo hakuzungumza katika eneo hili la viwanda, lakini balozi wa Tanzania nchini Rwanda, Ernest Jumbe Mangu, amesema ushirikiano wa nchi mbili ni wa lazima:
Baadaye Rais Samia Suluhu Hassan amerejea nyumbani saa nane za mchana majira ya Rwanda baada ya kuikamilisha ziara hiyo ya siku mbili.
Sylvanus Karemera/DW Kigali