1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Samia ziarani Urusi

3 Juni 2026

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameanza ziara ya kitaifa ya siku tatu Urusi, ambapo anatarajiwa kukutana na Rais Vladmir Putin katika wakati ambapo sifa ya Tanzania inazidi kuchafuka kwenye nchi za Magharibi.

Nairobi, Kenya 2022 | Rais Samia Suluhu Hassan
Ziara ya Rais Samia nchini Urusi kuimarisha uhusiano wa nchi hizo mbiliPicha: Billy Mutai/AA/picture alliance

Rais Putin atamkaribisha Rais Samia siku ya Jumatano katika Ikulu ya Urusi, Kremlin, kabla ya kuhudhuria Jukwaa la Kimataifa la Uchumi huko St. Petersburg. Ziara hiyo inalenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, kisiasa, kiuchumi, na kihistoria kati ya mataifa hayo mawili.

Hata hivyo, ziara hiyo inafanyika wakati ambapo wanadiplomasia na mashirika ya kutetea haki za binaadamu yakiishutumu serikali ya Rais Samia kwa mauaji ya mamia ya watu wakati wa ghasia za uchaguzi mkuu wa Oktoba, 2025, pamoja na utekaji nyara na mauaji dhidi ya wakosoaji katika kipindi cha kuelekea kwenye uchaguzi huo.

Uhusiano wa kidiplomasia na nchi za Magharibi

Marekani imesema inapitia upya uhusiano wake na Tanzania kutokana na ghasia hizo, na wiki iliyopita ilimuwekea vikwazo afisa wa ngazi ya juu wa polisi kutokana na kuwatesa wanaharakati wawili maarufu.

Kwa upande mwingine, Rais Putin, alikuwa mmoja wa viongozi wa kwanza wa nchi kumpongeza Rais Samia kwa kushinda katika uchaguzi huo kwa asilimia 98.

Rais Putin kukutana na Rais Samia katika Ikulu ya KremlinPicha: Alexander Shcherbak/TASS/ZUMA/picture alliance

Uhusiano kati ya nchi hizo mbili umekuwa ukiimarika tangu wakati huo. Baraza la Biashara kati ya Urusi na Tanzania lilianzishwa mwezi Januari na mwezi uliopita wa Mei, Shirika la Ndege la Tanzania lilitangaza kuanzisha safari zake za ndege kutoka Dar es Salaam hadi Moscow, ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

Rais Samia hajaomba radhi wazi wazi kuhusu ukandamizaji wa kisiasa nchini Tanzania, na badala yake amekuwa akiwaelezea wanaharakati hao na waandamanaji kama "watoto wasio na heshima" ambao wanapaswa "kuchapwa viboko".

Mikataba kadhaa kusainiwa

Katika ziara yake hiyo, Rais Samia ameongozana na ujumbe wa wafanyabiashara akiwa na matumaini ya kuimarisha mikataba ya kibiashara, utalii na madini.

Hii ni ziara ya pili kufanywa na Rais wa Tanzania nchini Urusi, baada ya ile iliyofanywa na Baba wa Taifa, Rais Julius Kambarage Nyerere, Oktoba waka 1969.

Maandamano ya wakati wa uchaguzi wa Oktoba, 2025Picha: AFP

Biashara kwa sasa inafikia zaidi ya dola milioni 307 kwa mwaka, na mradi pekee wa pamoja ni madini ya urani ambao umekuwa ukipangwa kwa zaidi ya muongo mmoja.

Aliyekuwa Profesa wa Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambaye hakutaka kutajwa jina kutokana na ukandamizaji unaoendelea nchini Tanzania, anasema Urusi inaweza kutumia uungwaji mkono huo hata kama ni kwa ajili ya kujizuia kupiga kura muhimu katika Umoja wa Mataifa kuhusu vita vya nchini Ukraine.

Urusi kutumia udhaifu wa Tanzania

Aidha, Fergus Kell, wa Taasisi ya Uingereza ya Chatham House, anasema kuwa Urusi inaweza ikawa inatumia fursa ya utawala dhaifu wa Tanzania.

Ripoti ya serikali kuhusu ghasia za uchaguzi wa mwaka uliopita, ilieleza kuwa watu 518 waliuawa, lakini haikusema nani aliyehusika na mauaji hayo, na hakuna watu waliowajibishwa hadi sasa.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW