1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Sarkozy azuru Urusi

Charo, Josephat8 Septemba 2008

Viongozi wa Umoja wa Ulaya watarajiwa kuishinikiza Urusi iondoe majeshi yake kutoka Gerogia

Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy (kushoto) na rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jose Manuel Barroso.Picha: AP

Rais wa Ufaransa Nicholas Sarkozy leo anaitembelea Urusi na Georgia katika juhudi za kuongeza shinikizo la kimataifa dhidi ya Urusi na kuitaka iondoe majeshi yake kutoka Georgia. Kiongozi huyo pia ataitaka Urusi iheshimu mkataba wa kusitisha mapigano na kujadili uhusiano kati ya Urusi na Umoja wa Ulaya.

Rais wa Ufaransa Nicholas Sarkozy ambaye pia ni mwenyekiti wa Umoja wa Ulaya anatarajiwa kukutana na rais wa Urusi, Dmitry Medvedev katika ikulu ya mjini Moscow hii leo. Katika ziara yake hiyo rais Sarkozy ameandamana na rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya, Jose Manuel Barroso na kiongozi wa sera za kigeni wa umoja huo, Javier Solana. Licha ya mzozo kati ya Urusi na Georgia, Solana anasema nchi 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya zinataka kuendeleza mazungumzo na serikali ya Moscow kutafuta suluhisho la kudumu.

´´Nadhani tumepiga hatua mbele kuelekea njia inayofaa kwa kuendelea kuweka wazi njia za mawasiliano na Urusi kama nchi muhimu. Na tuna matumaini makubwa kwamba mazungumzo ya mjini Moscow yataturuhusu kuendelea kufanya kazi pamoja´´

Ziara ya viongozi wa Umoja wa Ulaya nchini Urusi ni juhudi mpya inayolenga kuifafanulia Urusi msimamo wa umoja huo kuhusiana na mzozo wa eneo la Caucasus. Rais Sarkozy amesema hatua ya Urusi kuishambulia Georgia kijeshi na kutaka kuikalia haikubaliki.

´´Hatua ya Urusi kuichukulia Georgia hatua za kijeshi zilizovuka mpaka na kutambua uhuru wa majimbo ya Georgia yaliyojitenga ya Ossetia Kusini na Abkhazia imezusha wasiwasi mkubwa barani Ulaya. Kurejea kwa siasa ya kuwa na maeneo ya ushawishi hakuwezi kukubalika.´´

Maafisa wa Ufaransa wamesema rais Sarkozy atamtaka rais wa Urusi Dmitry Medvedev aweke tarehe ya kuwaondoa wanajeshi wote wa Urusi walio nchini Georgia na kupelekwe tume ya waangalizi wa Umoja wa Ulaya nchini Georgia. Rais Sarkozy pia atataka kufanyike mazungumzo ya kimataifa kuhusu mustakabali wa majimbo ya Georgia yaliyojitenga ya Ossetia Kusini na Abkhazia.

Swala lengine muhimu litakalojadiliwa katika ziara ya viongozi wa Umoja wa Ulaya mjini Moscow ni hali ya baadaye ya uhusiano kati ya umoja huo na serikali ya Urusi. Umoja wa Ulaya hautafanya mazungumzo yoyote ya ushirikiano wa kimkakati na Urusi mpaka nchi hiyo iondoe majeshi yake kutoka Georgia. Mazungumzo kuhusu mkataba mpya kati ya pande hizo yalianza tena mwezi Juni mwaka huu baada ya kuahirishwa kwa muda mrefu. Hata hivyo balozi wa Urusi katika Umoja wa Ulaya, Vladamir Tschischow, anasema Urusi bado ina matumaini.

´´Hata hivyo kuhusu kasi ya mazungumzo tumekuwa wavumilivu. Tunayahitaji sana mazungumzo haya kama vile Umoja wa Ulaya unavyoyahitaji.´´

Rais Nicholas Sarkozy, Jose Manuel Barosso na Javier Solana wanatarajiwa leo m chana kwenda mjini Tbilisi Georgia ambako watafanya mazungumzo na rais wa nchi hiyo Mikheil Saakashvili, ambaye Urusi imekataa kuzungumza naye ana kwa ana.