Rais Sarkozy wa Ufaransa azuru India
25 Januari 2008Rais wa Ufaransa Nicoals Sarkozy ameanza ziara ya siku mbili nchini India hii leo. Kiongozi huyo ameandamana na maafisa wa serikali yake katika ziara inayolenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kisiasa kati ya India na Ufaransa.
Rais Sarkozy atakuwa mgeni wa heshima kwenye sherehe za kuadhimisha sikukuu ya jamhuri ya India hapo kesho.
Kiongozi huyo amesema Ufaransa na India zinakaribia kufikia makubaliano kuhusu maswala ya nishati ya nyuklia kwa ajili ya matumizi ya kiraia. Makubaliano hayo hata hivyo yatasainiwa wakati India itakapokamilisha masharti ya shirika la kimataifa la kuzuia utapakazaji wa silaha za kinyuklia, IAEA, kutoa maelezo ya kina kuhusu mpango wake wa nyuklia.
Mkataba huo pia utatakiwa uidhinishwe na kundi la nchi zinazomiliki teknolojia ya nyuklia.
Rais Sarkozy amesema anaunga mkono mkataba ulio na utata kuhusu nyuklia kati ya Marekani na India na pia akadokeza kuhusu msimamo wa Uingereza kuiunga mkono India katika juhudi zake za kutaka kiti cha kudumu katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.