1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Steinmeier amwagia sifa waziri mkuu Ethiopia

Oumilkheir Hamidou
29 Januari 2019

Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier akianza ziara ya siku nne nchini Ethiopia, ameahidi kuunga mkono juhudi za mageuzi katika nchi hiyo ya mashariki mwa Afrika.

Deutschland Bundespräsident Steinmeier zu Staatsbesuch in Äthiopien
Rais Frank-Walter Steinmeier akisalimiana na waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed Ali baada ya rais Steinmeier kumtemebelea ofisini kwake mjini Addis Ababa.Picha: Office of the Prime Minister Ethiopia 

"Nimefika katika nchi iliyobadilika, nchi inayochipuka. Nchi inayofanyiwa mageuzi. Kwa niaba ya wote niliofuatana nao, naamini nnaweza kusema tuna fakhari na kusifu moyo wenu wa ujasiri wa kuanzisha mageuzi kama haya."

Amesema hayo rais wa shirikisho Frank-Walter Steinmeier baada ya mazungumzo pamoja na rais wa Ethiopia bibi Sahle-Work Zewde  mjini Addis Abeba.

Rais Steinmeier amekutana pia na waziri mkuu Abiy Ahmed anaewekewa matumaini makubwa na sio tu nchini Ethiopia.

Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 42 ndie aliyeanzisha mageuzi hayo makubwa tangu April mwaka 2018. Amewaachia huru maelfu ya wafungwa wa kisiasa na kuanzisha mfumo wa kiliberali wa kiuchumi.

Waziri mkuu Abiy Ahmed amefikia makubaliano ya amani pamoja na nchi jirani ya Eritrea wanakotokea wakimbizi wengi wanaoingia Ujerumani. Amefanikiwa pia kuleta wezani wa kijinsia katika nyadhifa za serikali.

Rais Frank-Walter Steinmeier alipopokelewa na rais wa Ethiopia Sahle-Work Zewde, Januari 28.01.2019.Picha: DW/L. Schadomsky

Changamoto bado zipo lukuki

Hata hivyo bado mivutano ya kikabila inatishia umoja wa nchi hiyo. Umaskini na ukosefu wa ajira ni wa hali ya juu.

Ethiopia inakabiliwa na changamoto kubwa-kisiasa, kiuchumi na kijamii, amesema rais Steinmeier aliyehakikisha ni kwa masilahi ya Ujerumani kuona mageuzi yanafaana na kuahidi Ujerumani itasaidia kwa uwezo wake wote mageuzi nchini Ethiopia.

"Nuru ya mapambazuko ya kidemokrasi inaweza kunawiri mpaka nje ya Ethiopia hadi barani Ulaya na kwa namna hiyo kuibadilisha pia picha ya Afrika barani Ulaya, picha inayoliangalia bara la Afrika kuwa ni bara la mizozo na mivutano.

Ujumbe wa wanauchumi unafuatana na rais Steinmeier katika ziara yake hii ya siku nne nchini Ethiopia. Jumatatu jioni rais Steinmeier na ujumbe wake wamepangiwa kutia saini waraka wa ushirikiano kati ya kampuni ya Volkswagen na tume ya  vitega uchumi ya Ethiopia. Lengo ni kubuni chombo cha usafiri kwaajili ya nchi hiyo yenye wakaazi milioni 100.

Rais Steinmeier amepangiwa kukutana na viongozi wa Umoja wa Afrika siku ya Jumatano.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/dpa

Mhariri: Grace Patricia Kabogo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW