1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Rais Trump aanza awamu mpya kwa kishindo

20 Januari 2025

Rais wa Marekani Donald Trump ameanza awamu ya pili ya urais leo Jumatatu, wakati ulimwengu ukijiandaa na kurejea kwa kiongozi huyo asiyetabirika.

Marekani, Washington 2025 | Donald Trump akiapa kuwa rais
Rais wa 47 wa Marekani Donald Trump akila kiapo cha urais katika ukumbi wa Capitol Hill, mjini Washington, Januari 20, 2025Picha: Morry Gash/REUTERS

Rais Trump amekula kiapo majira ya mchana ya Marekani na kuanza kazi mara moja. Lakini baada ya kuapishwa, Trump ambaye ni rais wa 47 wa Marekani alitoa hotuba iliyojaa ahadi za kila aina, na kusema enzi ya Dhahabu nchini humo ndio inaanza sasa.Donald Trump anatarajiwa kuapishwa hii leo kuwa Rais wa 47 wa Marekani

Bila ya kumtaja mtangulizi wake Joe Biden, Trump alitaja msururu wa maagizo ya rais aliyosema atasaini mara baada ya shughuli ya kiapo, na kuahidi kuinusuru Marekani dhidi ya ''miaka ya kusalitiwa na kudidimizwa.''

Trump, katika hotuba hiyo alisema atachukua hatua kali dhidi ya wahamiaji haramu huku akijinasibu yeye mwenyewe kama mkombozi wa taifa hilo aliyechaguliwa na Mungu. "Kwa raia wa Marekani, Januari 20 ni Siku ya Ukombozi", alisema Trump.

Trump atumia hotuba yake kuikosoa serikali iliyopita

Wakati akijitanabahisha kama mtu wa amani na mpatanishi, hotuba yake imechukua sura ya kichama badala ya kitaifa, tofauti na za marais waliotangulia. Trump mwenye umri wa miaka 78 alitoa shutuma kali dhidi sera za mtangulizi wake Biden aliyekuwa amekaa pembeni yake, akianzia ile ya uhamiaji hadi yamambo ya nje.

Wahamiaji kutoka jimbo la Tapachula, Chiapas nchini Mexico wakielekea kwenye mpaka na Marekani, Januari 20, 2025. Rais Donald Trump amesema atachukua hatua kali dhidi ya uhamiaji haramu Picha: Isaac Guzman/AFP

Aidha, ameutaja msururu wa amri za rasi anazotarajia kuzitia saini mara moja baada ya kula kiapo, ikiwa ni pamoja na kutangaza dharura ya kitaifa kwenye mpaka kati ya Marekani na Mexico pamoja na kupeleka wanajeshi kwenye eneo hilo.

"Kwanza, nitatangaza dharura ya kitaifa kwenye eneo la kusini la mpaka wetu," alisema Trump na kuongeza kuwa ''uhamiaji haramu utamalizwa mara moja, na tutaanza mchakato wa kuwarejesha makwao mamilioni kwa mamilioni ya wageni wahalifu."

Trump hali kadhalika ameahidi kubadilisha jina la Ghuba ya Mexico na kuwa Ghuba ya Marekani, huku akirudia tena azma yake ya kuchukua udhibiti wa Mfereji wa Panama, moja ya sera zake za kigeni, ambayo imeibua mshangao miongoni mwa washirika wa Marekani.

Serikali mpya yalenga kupunguza mfumuko wa bei

Ameahidi pia kusaini mkataba utakaoangazia mkakati kabambe wa serikali katika kupunguza mfumuko wa bei, ingawa amejizuia kwa sasa kuzungumzia tena kitisho cha kuziwekea ushuru China, Mexico, Canada na nchi zingine.

Rais huyo mpya aidha amesema atatangaza dharura ya kitaifa ya nishati inayolenga kuimarisha uzalishaji wa taifa hilo wa mafuta na gesi, ili kupunguza gharama kwa watumiaji nchini humo.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ni mmoja ya viongozi wa mwanzo kumpongeza Rais Donald Trump wa Marekani, akisema yuko tayari kushirikiana nayePicha: Uncredited/Israeli Government Press Office/AP/dpa/picture alliance

"Marekani kwa mara nyingine litakuwa taifa linalozalisha kiviwanda, na tuna kitu ambacho mataifa mengine wazalishaji hawatawahi kuwa nacho, kiwango kikubwa kabisa cha mafuta na gesi kuliko taifa lolote duniani, na tutayatumia," alisema Trump.

Biden atoa hotuba ya kuaga na kuelezea wasiwasi wake kuhusu utawala ujao wa Trump

Hatua hii itageuza kabisa juhudi za awali zilizochukuliwa na mtangulizi wake zilizolenga kuviimarisha zaidi viwanda vinayozalisha magari ya umeme.

Viongozi mbalimbali wamempongeza Trump kwa kurejea kwake Ikulu ya White House. Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amempongeza kupitia video iliyochapishwa kwenye mtandao wa X, akisema "Mimi na Sara tunakupongeza sana, wewe, Melania na watu wa Marekani kwa kurejea kwa mara ya pili kama rais wa Marekani."

Soma pia:Hafla ya kuapishwa Trump kufanyika ndani ya jengo la Bunge

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi pia amempongeza Trump kwa kurejea madarakani akiandika kupitia X "mpendwa rafiki" Donald Trump ninataraji kushirikiana na wewe kwa karibu na kuitengeneza dunia, kwa ajili ya mustakabali bora ujao."

Rais wa Ukraine, Volodymyy Zelensky pia amempongeza Trump akisema "Leo ni siku ya mabadiliko na pia ni siku ya matumaini kuelekea suluhu ya matatizo mengi, ikiwa ni pamoja na changamoto za kiulimwengu," aliandika Zelenksy kwenye ukurasa wa X.

Sikiliza pia:

Wamarekani wanatarajia nini kutoka kwa Trump?

This browser does not support the audio element.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW