1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Trump akiri Jamal Kashoggi huenda akawa amefariki

19 Oktoba 2018

Rais wa Marekani Donald Trump amekiri huenda mwaandishi habari wa Saudi Arabia Jamal Kashoggi amefariki na kutishia kuchukuwa hatua kali iwapo itathibitika viongozi wa Saudi Arabia walihusika na kifo chake.

USA Präsident Trump spricht vor Anhängern über die Berufung von Kavanaugh an den Obersten Gerichtshof
Picha: Reuters/Y. Gripas

Onyo la Rais huyo wa Marekani limekuja wakati serikali yake ikizidisha ukali juu ya kupotea kwa Mwaandishi Habari Jamal Khasoggi kulikoibua ghdhabu ya Kimataifa. Trump amesema kwa sasa wanasubiri majibu ya uchunguzi kabla ya kutoa taarifa ya aina yoyote.

Kabla ya Trump kuzungumza siku ya Alhamisi utawala wake ulitangaza kuwa waziri wake wa fedha Steven Mnuchin amejiondoa kwenye mkutano mkubwa wa uwekezaji unaoandaliwa na Saudi Arabia. 

Mwanahabari Jamal KhashoggiPicha: picture-alliance/AP Photo/V. Mayo

Wakati huo huo aafisa wa Marekani wakisema kuwa Waziri wa mambo ya kigeni Mike Pompeo alimuonya mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman kuwa uaminifu wake kama kiongozi wa siku za usoni wa taifa hilo uko mashakani.

Pompeo amesema Saudi Arabia inapaswa ipewe muda wa siku chache zijazo wa kufanya uchunguzi wa wazi na unaoaminika kabla Marekani haijaamua namna na vipi itakavyojibu.

Tamko la Rais wa Marekani Donald Trump linatoa ishara ya haja ya kuongeza kasi katika uchunguzi juu ya kupotea kwa mwanahabari Jamal Kashoggi.

Kashoggi alieonekana mara ya mwisho tarehe 2 Oktoba alipokuwa akiingia katika ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul, nchini Uturuki. Kashoggi alikuwa mkosoaji mkubwa wa mwanamfalme Muhammed Bin Salman.

Rais Donald Trump wa Marekani na Mwanamfalme Mohammed bin Salman wa Saudi ArabiaPicha: picture-alliance/AP Photo/E. Vucci

Huku hayo yakiarifiwa wachunguzi wa Uturuki wameanzisha msako katika misitu mjini Istanbul kama njia moja ya uchunguzi wao juu ya kupotea kwa mwanahabari huyo.

Duru kutoka Uturuki zinadai kuwa mwanahabari Jamal Khashoggi, aliingizwa katika ubalozi huo na kuuwawa.

Maafisa wa Saudi Arabia wanasema kuwa aliondoka ubalozini humo lakini hawajatoa ushahidi wa kuthibitisha madai hayo.

Saudi Arabia ni moja ya washirika wa karibu wa Marekani wenye nia ya kuikandamiza Iran. Saudi pia ni mteja muhimu katika sekta ya silaha za Marekani.

Mwandishi Amina Abubakar/AP/AFP

Mhariri: Iddi Ssessanga

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW