1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatimaye Trump asaini muswada wa misaada ya COVID-19

Sylvia Mwehozi
28 Desemba 2020

Rais wa Marekani Donald Trump ameusaini muswada wa sheria wa dola bilioni 900, unaokusudia kutoa misaada kwa watu walioathiriwa na janga la virusi vya corona

USA Präsident Donald Trump
Picha: Tom Brenner/REUTERS

Kwa siku kadhaa rais Trump alikataa kutia saini muswada huo tangu ulipopitishwa wiki iliyopita na bunge akiutaja kuwa fedheha. Kulikuwa na wasiwasi kwamba kuchelewa kufanya hivyo, kungesababisha baadhi ya faida za ukosefu wa ajira kupotea, ikimaanisha kwamba mamilioni ya watu wangeweza kupoteza pesa wakati huu mgumu wa uchumi uliochangiwa na janga la virusi vya corona.

Mpango huo unaotoa misaada ya dharura ya janga la virusi vya corona, ni sehemu ya muswada mkubwa wa matumizi ambao pamoja na saini ya Trump, utasaidia kuepusha shughuli za serikali kufungwa. "Ninasaini muswada huu kurejesha manufaa ya ukosefu wa ajira, kuzuia watu kuondolewa kwenye nyumba, kutoa misaada, kuongeza pesa katika programu za ulinzi wa malipo, kurudisha wafanyakazi wetu wa ndege kazini, kuongeza pesa zaidi katika usambazaji wa chanjo na mengi zaidi", alisema Trump katika taarifa yake wakati wa mapumziko ya Krismasi huko Florida.

Picha: Saul Loeb/AFP/Getty Images

Hatua ya Trump kubadili msimamo imekuja baada ya simu kutoka pande zote za kisiasa za kumtaka achukue hatua za kuepusha maafa ya kiuchumi na kijamii, hasa kwa wamarekani wengi walio katika mazingira magumu. Programu mbili za manufaa ya ukosefu wa ajira zilizoidhinishwa mwezi Machi, kama sehemu ya mpango wa awali wa misaada ya covid-19 zilimalizika usiku wa Jumamosi na kuibua wasiwasi kwa wamarekani wengi.Marekani kuanza kutoa chanjo ya COVID-19 Jumatatu

Seneta wa Republican mwenye ushawishi Mitt Romney amesema amesema amefarijika baada ya rais Trump kutia saini, akiongeza kwamba sasa misaada iko njiani kuwafikia wafanyakazi, familia na wafanyabiashara ndogo kote nchini ambao wana uhitaji mkubwa.

Mpango huo mpya unatoa misaada ya shirikisho kwa wasio na kazi hadi katikati ya mwezi Machi, na kutoa mikopo ya uhakika na mabilioni ya dola kusaidia wafanyabiashara wadogo, migahawa, hoteli, mashirika ya ndege na kampuni zingine. Mpango huo ni muhimu kwa taifa hilo kubwa kiuchumi ambalo limeathiriwa sana na janga la virusi vya corona. Kiongozi wa Democratic bungeni Nancy Pelosi, ameuita muswada huo kuwa malipo ya chini kwa kile kinachohitajika kukabilina na kirusi hicho akiongeza kuwa "lazima kuchukuliwe hatua zaidi na haraka".

Trump amesisitiza kwamba malipo ya moja kwa moja yaongezwe kutoka dola 600 katika muswada hadi dola 2000. Baraza la wawakilishi litapiga kura kuongeza kiwango hicho kwa mtu mmoja mmoja.