Rais Tshisekedi asema Rwanda inaendesha "vita ya kiuchumi"
18 Juni 2022Shirika la Habari la Associated Press limenukuu rais Tshisekedi akisema hali ya usalama mashariki mwa Congo inaendelea kuzorota kwa sababu Rwanda inajaribu kudhibiti sehemu ya ardhi ya Congo yenye utajiri wa madini ya dhahabu na kobalti kwa manufaa yake.
Tshisekedi amesema kinachoendelea ni vita ya kiuchumi ya kuwania rasimali na Rwanda inayatumia magenge yake ya kigaidi.
Hapajawa na majibu yoyote kutoka nchini Rwanda kuhusiana na matamshi hayo ya Tshisekedi, ingawa Rwanda mara kadhaa imekanusha madai ya kuwaunga mkono waasi wa M23 ambao waliukamata mji muhimu mashiriki mwa Congo mapema wiki hii.
Kwenye matamshi yake rais Tshisekedi amewataka viongozi wa kimataifa ikiwemo waziri mkuu wa Uingereza kuikosoa Rwanda bila kificho pindi watakapohudhuria mkutano wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Madola baadae wiki ijayo mjini Kigali. "Raia wa mashariki mwa DRC hawana hatia lakini wanashambuliwa na jirani yetu" amesema Tshisekedi.
Matamshi ya kiongozi huyo huenda yatachochea moto kwenye mzozo unaotanuka baina ya mataifa hayo jirani ya eneo la maziwa makuu.
Mwanajeshi wa Congo ajeruhi wawili naye auliwa upande wa Rwanda
Tayari mvutano umefikia kiwango cha kutia wasiwasi. Siku ya Ijumaa Jeshi la Rwanda lilisema kuwa mwanajeshi mmoja wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo aliyebeba bunduki aina ya AK-47 alivuka mpaka na kuwafyatulia risasi polisi wa Rwanda, kabla ya mwanajeshi huyo kupigwa risasi na kuuawa.
Taarifa hiyo ilisema polisi wawili wa Rwanda walijeruhiwa katika shambulizi hilo lililotokea kwenye kivuko kidogo cha mpakani kijulikanacho kama Petite Barriere. Msemaji wa serikali ya Kongo amethibitisha kisa hicho, lakini hakutoa maelezo zaidi.
Wakati huo huo duru kutoka mashariki mwa Kongo zimearifu kuwa waasi wa M23 wameudhibiti mji mwingine wa Tshengerero, ulio mashariki mwa Bunagana, mji wa kimkakati kwenye mpaka kati ya Kongo na Uganda, ambao uliangukia mikononi mwa M23 mapema wiki hii.
Afisa wa shirika la kiraia ambaye hakutaka jina lake litajwe, amelithibitishia shirika la habari la Reuters taarifa hizo, akisema mamia ya wapiganaji wa M23 walikuwa wameenea kila mahali.
Malengo ya M23 ni kuukamata mji wa Goma
Katika hatua nyingine wataalamu huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo walisema siku ya Ijumaa kuwa waasi wa M23 walipanga kuukamata mji wa Goma ili kuishinikiza serikali ya Kinshasa kuridhia matakwa yao ya kisiasa.
Jumatatu wiki hii waasi wa M23 waliukamata mji wa kimkakati wa Bunagana ulio kwenye mpaka baina ya Kongo na Uganda.
Ripoti ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa iliyoandikwa tarehe 14 Juni na kuchapishwa Ijumaa, imesema malengo ya waasi hao ni kuuzingira mji wa Goma, ili baadaye waweze kuukamata.
Mji wa Goma wenye wakaazi wapatao milioni moja, ni makao makuu ya mkoa wa Kivu Kaskazini, na ni kituo kikuu cha biashara kwenye mpaka kati ya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.