Rais Tshisekedi kuuvunja ushirikiano na upande wa Kabila
7 Desemba 2020Ushirikiano huo umekuwa ukiongoza serikali ya Kongo kwa miaka miwili iliyopita, Kabila akilidhibiti bunge, huku Tshisekedi akiwa na mamlaka ya rais. Uamuzi huo Tshisekedi ameutoa katika hotuba kwa taifa jana Jumapili.
Hotuba yake rais Tshisekedi ilikuwa ikisubiriwa kwa shauku, baada ya mazungumzo ya mashauriano aliyoyafanya mwezi novemba, kwa kile kilichoelezewa kuwa lengo la kuunda muungano wa taifa.
Soma pia: Mzozo wa kisiasa DRC wazidi kuibua wasiwasi
Katika hotuba hiyo, Tshisekedi ameyagusia masuali mengi ambayo amesema yalijitokeza katika mazungumzo hayo, la muhimu zaidi likiwa ni hatua za kuhitimisha ushirikiano baina ya muungano wa vyama vinavyomuunga mkono yeye, maarufu CACH, na ule wa vyama vilivyo upande wake rais mstaafu Joseph Kabila yaani FCC.
Je wachambuzi walizungumziaje suala hili? Sikiliza mahojiano.
"Nimeamua kumaliza ushirikiano kati ya FCC na CACH. Hatua hiyo ya ya kusikitisha imekuja baada ya kujaribu muda wa miaka miwili, kusubiri na kuvumilia ili kuunusuru ushirikiano huo. Miaka miwili ya juhudi ila kwa kweli, hatukufaulu kuepuka hali ya vurugu iliyodumu." Amesema Rais Tshisekedi.
Mpasuko mkubwa muungano wa Tshisekedi, Kabila Congo
Baada ya hotuba ya rais Tshisekedi, wafuasi wake walijimwaga barabarani ili kusherehekea kumalizika kwa ushirikiano baina yamiungano hiyo ya kisiasa.
"Mimi ni miongoni mwa waliokuwa wakisubiri hatua hiyo. Mimi ni kijana mkongomani msomi, ila sina kazi. Ndoto yetu ilikuwa kutoka katika hali hiyo kwani ushirikiano huo haukutusaidia kitu. Tulikuwa tumechoshwa na ushirikiano huo. Sasa binafsi, naona kiongozi wa taifa tayari amejikomboa." Amesema Eli Okitawao ambaye ni mmoja wa waandamanaji tuliozungumza nao.
Rais Tshisekedi ametangaza pia kwamba atamteua hivi karibuni, mjumbe atakaefanya utafiti wa chama au muungano wa vyama ulio na uwingi bungeni.
Lengo ni kujaribu kujipatia uwingi bungeni, waziri mkuu pia spika wa bunge watakaokuwa upande wake ili kumrahisishia utekelezaji mpango wake.
Lakini raia mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe anafikiri kwamba ni vigumu kwake Rais Tshisekedi kufaulu kwani tayari yupo katika shida.
"Ni vizuri ningoje aonyeshe wingi katika bunge. Bila hilo, ni vigumu tu kwani mpaka leo, hakuna hata kitu kimoja kinachotuonyesha kama kweli aliweza kuwashawishi wabunge kubadilisha kambi. Hakujakuwa uhakika kama aliweza kukutana na watu wakamuhakikisha sisi tutatoka ile ngambo na kuja kwako."
Wengi miongoni mwa wakongomani tuliokutana nawo wanawaza kwamba cha muhimu siyo kutangaza mwisho wa ushirikiano baina ya pande hizo mbili, ila wanachokisubiri ni matokeo ya hatua hiyo kuhusu faida ya wanainchi.