1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Rais Vladimir Putin ahitimisha mkutano wa kilele wa BRICS

25 Oktoba 2024

Rais Vladimir Putin wa Urusi amesema yuko tayari kuimarisha uhusiano na Marekani "ikiwa watakuwa tayari" kufanya hivyo.

Urusi | Vladimir Putin | BRICS
Rais wa urusi Vladimir Putin akizungumza katika Mkutano wa kilele wa kundi la BRICS aliouandaa huko Kazan, Oktoba, 2024Picha: Alexander Zemlianichenko/AFP

Rais Putin amesema hayo alipokuwa akihitimisha mkutano wa siku tatu wa kundi la BRICS huko Kazan nchini Urusi mapema leo Ijumaa.

"Itategemea namna Marekani itakacvyouchukulia uhusiano baina yetu baada ya uchaguzi. Ikiwa watakuwa tayari, nasi tutakuwa tayari. Na ikiwa hawataki, basi ni sawa," Putin alisema katika mkutano na waandishi wa habari.

Uhusiano kati ya Urusi na Marekani umedorora kufuatia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine mwaka 2022.

Lakini licha ya Urusi kutengwa kimataifa kutokana na uvamizi wake nchini Ukraine, kiongozi huyo wa Urusi Putin aliwakaribisha wawakilishi wa zaidi ya nchi 36 mjini Kazan wiki hii na kuwakutanisha wakuu wa nchi, ambao n pamoja na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi na Rais wa China Xi Jinping.

Soma pia:BRICS: Putin asema kuishinda Urusi ni ndoto isiyofikirika 

Kundi hilo linaibua kitisho kwa mataifa ya magharibi, wakati likitarajiwa kuwa mbadala wa utaratibu wa kiuchumi unaoongozwa na Marekani.

Rais Vladimir Putin aliwakutanisha wakuu mbalimbali wa nchi na wawakilishi kutoka mataifa 36 duniani kwenye mkutano wa BRICS huko Kazan, Oktoba, 2024Picha: Alexander Shcherbak/Tass/IMAGO

Putin anasema 'anakaribisha' juhudi za kumaliza vita nchini Ukraine

Alipoulizwa na waandishi wa habari jana usiku kuhusiana na ahadi ya mgombea wa urais nchini Marekani Donald Trump ya kusitisha mapigano nchini Ukraine, Putin alisema "Kile alichosema Trump hivi karibuni, nilichosikia, [ni] alizungumza kuhusu nia ya kufanya kila linalowezekana ili kumaliza mzozo nchini Ukraine, kwangu mimi nadhani ana nia ya dhati. Hakika tunakaribisha taarifa za aina hii, bila kujali ni nani anayezitoa," aliongeza.

Trump alipendekeza mwezi uliopita kwamba angeweza kusaidia kuleta suluhu ya kumaliza vita kati ya Urusi na Ukraine, huku akielezea mashaka yake kuhusu msaada wa Marekani kwa Ukraine.

Guterres asema uvamizi wa Urusi nchini Ukraine ni 'ukiukaji' wa mkataba wa Umoja wa Mataifa

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekutana na Rais Vladimir Putin wa Urusi na kumwambia uvamizi wake nchini Ukraine umekiuka sheria za kimataifaPicha: Alexander Nemenov/AFP/AP/dpa/picture alliance

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliyekwenda Urusi na kukutana na Putin kwa mara ya kwanza katika kipindi cha zaidi ya miaka miwili, amemwambia kiongozi huyo kwamba kuna haja ya kupatikana "amani ya haki" kulingana na Mkataba wa Umoja wa Mataifa, sheria za kimataifa na maazimio ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ili kumaliza vita nchini Ukraine.

Katibu Mkuu huyo alikutana na Putin pembezoni mwa mkutano huo wa BRICS, hatua iliyokosolewa vikali na Ukraine, iliyosema imekasirishwa kwa kuwa Guterres hakukubali mwaliko wa "mkutano wa Amani" wa Ukraine uliofanyika nchini Uswisi majira ya kiangazi.

Soma pia: Katibu Mkuu wa UN yuko Urusi kwa mkutano wa kilele wa BRICS

Mataifa ya BRICS yafikiria mfumo mbadala wa kifedha

Putin aidha alizishutumu nchi za Magharibi kwa kujaribu kuyakandamiza mataifa masikini na yanayoinukia kiviwanda kwa kuwawekea "vikwazo haramu vya upande mmoja,  ushawishi usio na kikomo wa kigeni kupitia kile wanachokielezea "kukuza demokrasia", haki za binadamu, na ajenda ya mabadiliko ya hali ya hewa."

Lengo moja kuu la mkutano huo lilikuwa ni kuongeza ushirikiano wa kiuchumi miongoni mwa wanachama wa BRICS, ikijumuisha njia mbadala za mifumo ya kifedha ambayo kwa sasa inatawaliwa na Magharibi.

"Lakini hatutengenezi mfumo wowote wa pamoja kwa sasa," Putin alisema. "Kile ambacho tayari tunacho kinatosha."

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW