Rais Volodymyr Zelensky kuzuru Marekani
21 Desemba 2022Ikulu ya Rais Joe Biden, imesema ziara hiyo inakusudia kuwasilisha ujumbe kwa Urusi kwamba nchi za Magharibi zimeungana na Ukraine.
Taarifa kutoka ikulu ya White House imesema Rais Joe Biden anatarajia kumlaki Rais Volodymyr Zelensky, kisha baadaye Zelensky atalihutubia bunge la Marekani, ikiwa ni hali ya kuonyesha mshikamano imara na Ukraine.
Rais Zelensky pia alithibitisha ziara hiyo yake kupitia ukurasa wake wa Twitter. Aliandika kwamba yuko njiani kuelekea Marekani, kuimarisha uthabiti na uwezo wa ulinzi wa Ukraine, na kwamba mazungumzo kati yake na Biden yatajumuisha pia ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.
Zelensky atembelea wanajeshi mstari wa mbele wa vita
White House imesema kwamba wakati wa ziara hiyo, Rais Biden atatangaza msaada mpya wa silaha kwa Ukraine kuisadia kujilinda dhidi ya uchokozi wa Urusi. Mapema siku ya Jumatano, afisa mmoja wa ngazi ya juu katika utawala wa Biden alisema msaada huo unakadiriwa kugharimu dola bilioni mbili.
Marekani kuipya Ukraine mfumo wa ulinzi wa Patriot
Kulingana na afisa huyo, msaada huo utajumuisha mfumo wa ulinzi aina ya Patriot. Amesema mfumo huo ni muhimu sana katika ulinzi wa miundombinu au mali ya Ukraine na watu wake dhidi ya mashambulizi ya kikatili yanayofanywa na Urusi kulenga miundombinu muhimu ndani ya Ukraine.
Kiev yashambuliwa kwa makombora ya Urusi
Afisa huyo ameongeza kuwa Marekani itatoa mafunzo kwa vikosi vya Ukraine kuhusu namna ya kutumia zana hizo.
Mfumo wa Patriot unaweza kuweka ulinzi dhidi ya mashambulizi ya ndege angani, dhidi ya makombora, dhidi ya ndege zinazoendeshwa bila marubani au hata roketi zinazofyatuliwa kutoka mbali.
Poland kuweka mifumo ya ulinzi ya Patriot kwenye ardhi yake
Wiki iliyopita, Urusi iliionya Marekani dhidi ya kuipa Ukraine mfumo wa Patriot. Msemaji wa wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi Maria Zakharova alisema, kama ilivyo zana nyingine nzito zinazopewa Ukraine, mfumo huo pia utalengwa kushambuliwa.
Tayari Marekani ilishaipa Ukraine makombora aina ya HIMARS na vilevile mifumo ya ulinzi wa ardhini NASAMS dhidi ya roketi, miongoni mwa zana nyingine.
Urusi yaanza mfululizo wa mashambulizi dhidi ya Ukraine
Ziara ya kwanza ya Zelensky tangu Urusi ilipoivamia Ukraine
Tangu Urusi ilipoivamia Ukraine Februari 24, Rais Zelensky hajawahi kuondoka nchini mwake. Badala yake, amekuwa akihudhuria mikutano mbalimbali ya kilele kwa njia ya video, na vilevile mawasiliano kwa njia ya simu kati yake na viongozi wenzake wa mataifa mengine.
Mnamo Jumanne, kwenye hotuba yake ya kila siku kwa raia wake kwa njia ya video, Zelensky alisisitiza kwamba ni muhimu sana kwa Ukraine kupita majira haya ya baridi kali hadi mwaka ujao na kupata mahitaji au msaada muhimu.
Siku ya Jumanne, Wademokrat na Warepublic nchini Marekani, walikubaliana juu ya muswada wa matumizi ya dola trilioni 1.7, ambayo kati yake dola bilioni 44.9 zitatengewa misaada kwa Ukraine.
Wafadhili wakutana Paris kusaidia Ukraine
Hata hivyo muswada huo unasubiri kupigiwa kura na baraza la seneti la Marekani na baraza la wawakilishi.
Spika anayeondoka wa bunge la wawakilishi Marekani Nancy Pelosi aliwahimiza wawakilishi kuhudhuria kikao cha Jumatano, alichokitaja kuwa spesheli kwa demokrasia. Hata hivyo hakutoa maelezo zaidi.
Dmitry Medvedev afanya ziara China
Katika tukio tofauti, rais wa zamani wa Urusi Dmitry Medvedev amefanya ziara ya kushtukiza nchini China na kufany amazungumzo na Rais Xi Jinping na kusema miongoni mwa yale waliyozungumzia ni mgogoro wa Ukraine.
Medvedev ambaye kwa sasa ni naibu mwenyekiti wa baraza la Usalama la Urusi ameongeza kuwa walijadilina vilevile kuhusu ushirikiano wa kimkakati kati ya Urusi na China, lakini hakutoa maelezo zaidi.
Vyanzo: DPAE, AFPE