Bolsonaro afukuza kazi watumishi wa serikai
4 Januari 2019Serikali ya Rais Jair Bolsonaro hapo jana imeanzisha kampeni ya kuwafuta kazi watumishi wa serikali ambao hawakubaliani na itikadi kali za siasa za mrengo wa kulia. Bolsonaro ameamuru kufukuzwa kazi kwa watu wapatao 300 waliokuwa na mikataba ya kazi ya muda.
Baada ya Bolsonaro kumaliza mkutano wake na baraza la mawaziri, mkuu wa shughuli za ikulu katika serikali hiyo mpya, Onyx Lorenzoni, amesema katika mkutano na waandishi habari kwamba uamuzi huo ndiyo njia pekee ya kutawala kwa mawazo yao, dhana zao na kufanya kile kinachotakiwa na walio wengi nchini Brazil. Lorenzoni anaangaliwa kama mtu mwenye mamlaka makubwa baada ya Bolsonaro.
"Tunahitaji, na tunao ujasiri wa kufanya kile ambacho serikali iliyomaliza muda wake tarehe 31 Desemba haikuweza kukifanya tangu mwanzo, kwa sababu ndiyo njia pekee tunaweza kuongoza kwa kutumia mitazamo yetu, dhana zetu na kufanya kile ambacho wengi katika jamii ya Brazil waliamua wanakitaka... Nacho ni kitu gani? Kuodoa kabisa mitazamo ya kisoshalisti na kikomunisti," amesema Onyx Lorenzoni.
Mbali na hilo, Bolsonaro aliyeapishwa Jumanne iliyopita amesema yuko tayari kufanya mazungumzo na Marekani ili iweze kufungua kambi ya kijeshi nchini Brazil katika siku za baadae.
Bolsonaro ameahidi muelekeo mpya wa uongozi kwa Brazil, ambao ni tofauti na ule wa miaka ya nyuma ya siasa za wastani na za mrengo wa kushoto. Ni vyama ambavyo vimekuwa vikitawala nchini humo tokea 1985 pale taifa hilo lilipoondokana na utawala wa kijeshi.
Bolsonaro arejesha urafiki wa Brazil na Marekani
Vyama hivyo pia vilikuwa vikitaka kuongoza kwa kujitegemea bila ya kuwa na ukaribu na Marekani, ambayo ilikuwa na ushawishi mkubwa katika eneo la Amerika Kusini wakati wa Vita Baridi.
Bolsonaro alimwambia Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo Jumatano iliyopita, kwamba sasa nchi zao zimekuwa marafiki. Na amethibitisha urafiki huo kwa kupinga uwekezaji wa China nchini Brazil pamoja na kukosoa utawala alioutaja kuwa wa mkono wa chuma wa siasa za mrengo wa kushoto nchini Venezuela, Cuba na Nicaragua.
Rais huyo mpya wa Brazil mwenye umri wa miaka 63, ni mtu anayemuunga mkono sana Rais wa Marekani Donald Trump. Alikuwa mjumbe wa baraza la Congress kwa miaka mingi, na alipata umaarufu kupitia kampeni yake ya uchaguzi iliyokuwa ikipinga ufisadi na kuunga mkono umiliki wa silaha. Kampeni yake ya uchaguzi ilifanikiwa kuwashawishi wafuasi wengi wa kihafidhina na wa siasa kali za mrengo wa kulia baada ya upande wa siasa za mrengo wa kushoto kushinda katika chaguzi nne mfululizo nchini humo.
Mwandishi: Yusra Buwayhid/afp/ap/DW
Mhariri: Mohammed Khelef