Rais wa Brazil Dilma Rousseff ajieleza baraza la Seneti
29 Agosti 2016Mbele ya baraza hilo Dilma amesema anajua kuwa atahukumiwa lakini dhamiri yake ni safi kwa kuwa amekuwa kiongozi mwaminifu katika kuliongoza taifa hilo kwa kufuata katiba kwa ajili ya maslahi ya taifa lake tangu alipochaguliwa tena kwa asilimia 54 ya kura mwaka 2014.
Baada ya kupata dakika 30 za kujieleza , Roussef alikuwa ajibu maswali kutoka kwa maseneta. Mchakato huo utahusisha tuhuma kwamba aliuvuruga uchumi wa Brazil kwa udanganyifu katika bajeti huku watetezi wake wakihoji kuwa analengwa tu na wabunge mafisadi.
Mchakato wa kumshitaki Roussef ulianza mnamo mwaka uliopita, wakati wapinzani ndani ya bunge walipowasilisha muswada wa kumuondoa madarakani. Utetezi wake unakuja siku moja au mbili kabla ya baraza la seneti kupiga kura juu ya iwapo kumvua urais au la.
Nje ya ukumbi wa seneti mamia ya wafuasi wa rais huyo wameonekana wakiendesha magari yao huku wakipiga kelele za kutaka kurudishwa madarakani pamoja na kuwa kuna matumani hafifu kwa Dilma kurejea katika nafasi hiyo. Mmoja kati ya watu wanaoumuunga mkono kiogozi huyo anasema
"Watu karibu milion 56 walimchagua kwa haki yao ya kupiga kura na sio hii serikali ambayo wanataka kutuweka tunamtaka Dilma tunamtaka Lula. Tunataka viongozi ambao wanawajali wabrazil, masuala ya njaana ambao wanajali kuhusu ukosefu wa fursa na elimu"
Michael Temer huenda akawa Rias wa nchi hiyo
Baada ya kusikilizwa kwa utetezi zoezi hilo linalotarajiwa kuendelea mpaka siku ya jumatano litakamilika kwa wabunge kupiga kura ambayo ndio hasa itaamua ambapo kunahitajika theluthi mbili ya wabunge wote kuweza kumtoa madarakani
Kwa upande mwingine Temer kiongozi wa mlengo wa kulia ambaye amekua akishika wadhifa wa urais wa nchi hiyo tangu kusimamishwa kwa rais Dilma anatumia vema kipindi hicho kujenga upya matumaini ya wananchi pamoja na kuwa anakutana na pingamizi hasa kuhusu uhalali wake kushika wadhifa huo.
Ikiwa Baraza la seneti litaridhia kumg'oa madarakani rais huyo Temer ataapishwa kuwa rais wa Brazil mpaka mwaka 2018 kutakapofanyika uchaguzi mkuu.
Mwezi May mwaka huu baraza la wawakilishi lilipiga kura 55 dhidi ya 22 kumsimamisha Rousseff kutoka wadhifa wake kwa siku 180
Uchumi wa Brazil ulishuka mpaka kufikia asilima 3.8 mwaka 2015 na kuna uwezekano ukashuka zaidi kwa asilima 3.3 mwaka huu ikiwa ni hali mbaya zaidi kuwahi kutokea tangu mwaka 1930
Mwandishi: Celina Mwakabwale
Mhariri:Iddi Ssessanga