1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Burundi afariki kwa mshtuko wa moyo

9 Juni 2020

Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza amefariki kwa ugonjwa wa moyo, serikali imetangaza siku ya Jumanne. Nkurunziza amefariki baada ya mteule wake, Evariste Ndayishimiye kushinda uchaguzi wa rais uliokumbwa na utata.

Präsident Burundis Pierre Nkurunziza
Picha: picture-alliance/dpa/B. Mugiraneza

"Burundi imempoteza mtoto wake wa kiume mwenye kustahili heshima, rais wa Jamhuri, kiongozi wa juu wa uzalendo wa taifa," msemaji wa serikali Prosper Ntahorwamiye katika taarifa.

Nkurunziza, alieongoza taifa hilo dogo la Afrika Mashariki kwa mihula mitatu, alikuwa anapanga kustafu siasa baada ya uchaguzi wa Mei.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Nkurunziza, 55, alihudhuria mechi ya mpira wa wavu siku ya Jumamosi mchana na alipelekwa hospitali jioni hiyo baada ya kuugua.

Ingawa alionekana kupata ahueni siku ya Jumapili na kuzungumza na waliokuwa wamemzunguka, hali yake ilizidi kuwa mbaya ghafla siku ya Jumatatu asubuhi.

Kisha akapata mshtuko wa moyo na licha ya juhudi za haraka kuustua, madaktari hakuweza kumsaidia. Alifariki katika hospitali ya Natwe Turashoboye, mkoani Karuzi, mashariki mwa Burundi.

Rais Nkurunziza akizungumza kwenye mkutano wa kampeni mkoani Gitega, katikati mwa Burundi, Aprili 27, 2020.Picha: picture-alliance/Photoshot/E. Ngendakumana

Serikali imesema kutakuwa na kipindi cha maombolezo cha siku saba kuanzia Jumanne na kwamba bendera zitapepea nusu mlingoti. Vitabu vya maombolezi vitakuwepo pia.

Utawala wake wa miaka 15

Nkurunziza aliingia madarakani mwaka 2005 baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyosababisha vifo vya karibu watu 300,000. Vita hivyo viliwapambanisha watu wa jamii ya kabila la Wahutu walio wengi, dhidi ya Watutsi wachache.

Makubaliano ya amani ya Arisha yaliweka viwango vya ugawanaji wa madaraka, kwa lengo la kuwalinda Watutsi. Katika miaka iliyofuatia hata hivyo, chama tawala - Baraza la Taifa la Ulinzi wa Demokrasia - Vikosi vya Ulinzi wa Demokrasia (CNDD-FDD) - kilikuwa kimejitenga na masharti ya makubaliano hayo.

Wakati Nkurunziza, ambaye ni Mhutu, alipotangaza mwaka 2015, uamuzi wake wa kuwania muhula wa tatu, licha ya ukomo wa mihula miwili uliowekwa na makubaliano hayo, machafuko ya kiraia yalizuka.

Ushindi wake katika uchaguzi ukasababisha mzozo uliopelekea mamia ya watu kuuawa na mamia kwa maelfu wakaikimbia nchi.

Utawala wa Nkurunziza umetawaliwa na matukio ya ukandamizaji wa vikosi vya usalama dhidi ya wapinzani na pia kuminya uhuru wa vyombo vya habari.Picha: picture alliance/dpa/D. Kurokawa

Utawala wake ulikuja kuelezwa kama wa ukandamizaji, ambapo Umoja wa Mataifa ulionya mwaka uliopita kwamba watu nchini Burundi walikuwa wanaishi chini ya utawala wa vitisho, hasa kueleka uchaguzi mkuu wa 2020.

Mabadiliko ya kikatiba yaliofanyika mwaka uliopita yaliidhinishwa ambayo yangemruhusu kusalia madarakani hadi 2034; lakini aliwashangaza wengi kwa kuamua kutogombea tena.

Hata hivyo, kueleka uchaguzi wa mwezi Mei, mashirika mbalimabali yaliorodhesha ukiukaji wa haki za binadamu uliofanywa na serikali yake, ikiwemo utekaji nyara, mateso, mauaji na unyanyasaji wa wapinzani na vyombo vya habari.

Muda mfupi kabla y auchaguzi Nkurunziza aliwakatalia waangalizi huru wa uchaguzi na kuwafukuza maafisa wa shirika la afya duniani (WHO), waliokuwa wnasaidia katika janga la covid-19.

Alipolegeza msimamo na kuruhusu waangalizi, aliwataka wabakie kwenye karantini, hatua iliyowafanya washindwe kutekeleza majukumu yao siku ya uchaguzi.

Nkurunziza mara kwa mara alitoa madai kwama Mwenyezi Mungu atawaokoa Waburundi kutokana na ugonjwa huo na aliruhusu matukio ya kidini, michezo na utamaduni kuendelea bila tahadhari yoyote.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW