1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Rais wa China ataka usawa katika usimamizi wa dunia

20 Aprili 2021

Rais Xi Jinping wa China amesema mfumo wa utawala wa kilimwengu lazima ufanywe uwe wa usawa na uadilifu zaidi, na kwamba kanuni zinazowekwa na nchi moja ama baadhi ya mataifa haziwezi kulazimishwa kufuatwa na wengine.

Virtueller G20-Gipfel | China
Picha: Rao Aimin/Xinhua/picture alliance

Akizungumza kwenye Jukwaa la Boao, ambalo ni mbadala na Jukwaa la Kiuchumi la Davos na lililo maalum kwa mataifa ya Asia, rais huyo wa taifa la pili kwa nguvu ulimwenguni amesema dunia inahitaji zaidi haki na sio utawala wa kundi ama nchi moja. 

Xi amewaambia washiriki wa jukwaa hilo kwamba kujenga vizuizi na kulazimisha mgawanyiko kutawaumiza watu wote na kamwe hakufaidishi hata mmoja. 

Bila ya kulitaja taifa lolote kwa jina, Rais Xi amesema kuwa dunia ya sasa inapaswa kukataa kurejea kwenye zama za vita baridi, huku akisema China itaendelea kupunguza orodha aliyoiita 'hasi' kwa ajili ya uwekezaji wa kigeni.

Kwa muda mrefu sasa, China imekuwa ikitaka kuweka mageuzi makubwa kwenye namna ulimwengu unavyosimamiwa, ikipigania mitazamo na maadili ya nchi nyingi nyengine kuakisika, yakiwemo ya China yenyewe, na sio mataifa machache yenye nguvu duniani. 

Mara kadhaa, Beijing imepambana na wadau wakubwa wa usimamizi wa ulimwengu, hasa Marekani, juu ya masuala kadhaa kuanzia ya haki za binaadamu hadi ushawishi wa kiuchumi wa China kwa mataifa mengine.

"Nchi kubwa ionekana kubwa kwa kuonesha kubeba wajibu mkubwa zaidi, na sio kuwalazimisha wengine waifuate." Alisema Rais Xi.

Marekani yaitenga China

Rais Joe Biden wa Marekani (kulia) anajaribu kuitenga China kwa kushirikiana na Japan.

Ijumaa iliyopita, Rais Joe Biden wa Marekani aliitisha mkutano wa kwanza wa kilele wa ana kwa ana na Waziri Mkuu wa Japan Yoshine Suga, ambapo China ilikuwa kwenye ajenda ya mwanzo kabisa.

Katika taarifa yao ya pamoja, viongozi hao wawili walisema wana wasiwasi mkubwa juu ya uvunjwaji wa haki za binaadamu katika jimbo Xinjiang la China na pia Hong Kong. 

Serikali ya Marekani inaishutumu China kwa kuendesha mauaji ya maangamizo dhidi ya Waislamu wa jamii ya Uighur kwenye jimbo la kaskazini la Xinjiang, madai ambayo China imekuwa ikiyakanusha.

Kama ishara ya wazi wa ushirikiano wa kiuchumi wa Marekani na Japan na katika kuitenga China, Biden alisema Marekani na Japan zitawekeza kwa pamoja kwenye miradi kama vile teknolojia ya mawasiliano ya 5G, maarifa ya kompyuta na biashara ya mitandaoni, maeneo ambayo China imeyahodhi vya kutosha. 

Mbali ya ushindani wa kijeshi kwenye Bahari ya Kusini ya China, Marekani inaikosowa China pia kwenye uzalishaji wa gesi zinachofua tabaka hewa na kutokuwa kwake tayari kushirikiana na mataifa mengine katika udhibiti wa athari za mabadiliko ya tabianchi yanayochochewa pakubwa na shughuli za viwandani za China.