1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaChina

Rais wa China Xi Jinping ailaani Marekani

7 Machi 2023

Rais wa China Xi Jinping amelaani kile alichokitaja kuwa ukandamizaji dhidi ya nchi yake unaoongozwa na Marekani huku akihimiza sekta ya kibinafsi ya nchi hiyo kuongeza uvumbuzi na kujitegemea zaidi

China Peking | Jiang Zemin Trauerfeier für Ex-Staats- und Parteichef | Xi Jinping
Picha: CCTV/AP/picture alliance

Katika ukosoaji nadra wa moja kwa moja kwa Marekani, Xi aliwaambia viongozi wa sekta ya viwanda ya China kwamba nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani, zimeweka vikwazo vya pande zote ikiwa ni pamoja na kuizingira na kuikandamiza nchi yao, na kusababisha changamoto kubwa zisizo za kawaida kwa maendeleo ya nchi hiyo. Xi, ambaye atashika muhula wa tatu mfululizo wa urais katika siku zijazo wakati wa mkutano mkuu wa chama cha kikomunisti, amesema kipindi cha miaka mitano iliyopita, kiligubikwa na vikwazo vipya ambavyo vinatishia kudhoofisha ukuaji wa uchumi wa China.

Xi aitaka China kuwa jasiri 

Shirika la habari la serikali la Xinhua, limesema kuwa katika hotuba kwa wajumbe wakati wa kongamano la ushauri wa kisiasa wa watu wa China (CPPCC) linaloendeshwa sambamba na NPC, Xi amesema kwamba China lazima iwe na ujasiri wa kupigana wakati taifa hilo linakabiliwa na mabadiliko makubwa na magumu katika mazingira ya ndani na ya kimataifa. Xi ameongeza kuwa kampuni za kibinafsi zinapaswa kuchukuwa hatua ya kuzingatia maendeleo ya kiwango cha juu.

Mapema wiki hii, Xi aliapa kuimarisha uwezo wa utengenezaji wa China na kusema nchi hiyo inapaswa kuwa na uwezo wa kujisimamia yenyewe. Kiongozi huyo ameongeza kuwa kila wakati amekuwa akisema kuna sehemu mbili muhimu kwa China ambazo ni kulinda raslimali zao na  kujenga sekta ya viwanda yenye nguvu.

Marekani imeimarisha vikwazo dhidi ya China

Waziri wa mambo ya nje wa China Qin GangPicha: Mark Schiefelbein/AP Photo/picture alliance

Katika miezi ya hivi karibuni, Marekani imeimarisha vikwazo dhidi China ikitaja masuala ya usalama wa kitaifa na athari ya teknolojia inayotumiwa na jeshi la China.

Wakati huo huo, waziri wa mambo ya nje wa China Qin Gang, amesema kuwa kile kinachoamua uhusiano kati ya China na Marekani kinapaswa kuwa maslahi ya pamoja, majukumu ya pamoja na urafiki kati ya mataifa haya mawili badala ya siasa za ndani za Marekani na shtuma za kiholela. Katika mkutano mrefu na wanahabari, Qin ambaye pia ni balozi wa zamani wa China kwa Marekani, alipuuzilia mbali tahadhari kutoka kwa mataifa ya Magharibi kwamba China huenda ikaisaidia Urusi na silaha kwa vita vyake nchini Ukraine akiongeza kwamba taifa lake halitakubali lawama, vikwazo, ukandamizaji na vitisho.

China yasema haitegemei upande wowote katika vita nchini Ukraine

Mwezi uliopita, China ilielezea msimamo wake kuhusu vita nchini Ukraine na kujielezea kama taifa lisiloegemea upande wowote huku ikizihimiza pande mbili katika vita hivyo kuingia katika mazungumzo ya amani. Hata hivyo, msimamo huo wa China umetiliwa shaka na Marekani na washirika wengine wa Ukraine  huku Urusi na China zikitaja uhusiano kati yao kuwa usiokuwa na mipaka, wiki mbili kabla ya uvamizi huo kutimiza mwaka mmoja.