China na Syria zatangaza ushirikiano mpya wa kimkakati.
22 Septemba 2023Shirika la habari la China CCTV limemnukuu Xi akisema ushirikiano huo mpya utakuwa hatua muhimu katika historia ya mahusiano ya nchi hizo mbili. Xi amsema wakati China ikikabiliwa na hali ya kimataifa iliyojaa ukosefu wa utulivu na uhakika, iko tayari kuendelea kushirikiana na Syria, kusaidiana, kukuza ushirikiano wa kirafiki na kwa pamoja kulinda haki na uadilifu wa kimataifa.
Soma pia:Maandamno Syria: Mapinduzi mapya au masuala ya kiuchumi?
Xi amesema uhusiano kati ya mataifa hayo mawili umestahimili mabadiliko ya kimataifa na kwamba urafiki kati ya mataifa hayo umeimarika kwa muda.
China yasema uhusiano kati yake na Syria umedumisha maendeleo bora na thabiti
Alhamisi (21.09.2023) msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Mao Ning alisema ziara ya Assad inatilia maanani kukuwa kwa uhusiano kati ya China na Syria. Mao Ning ameongeza kuwa tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia miaka 67 iliyopita, uhusiano kati ya China na Syria umedumisha maendeleo bora na thabiti.
Assad anatafuta msaada wa kifedha kuijenga upya Syria
Ziara ya Assad iliyoanza jana Alhamisi ni ya kwanza rasmi nchini China katika muda wa takriban miongo miwili huku akitafuta msaada wa kifedha kusaidia kuijenga upya nchi yake iliyoharibiwa na vita. Assad pia atahudhuria hafla ya ufunguzi wa michezo ya 19 ya Asia huko Hangzhou hapo kesho Jumamosi.
Soma pia:Mapigano Kaskazini Mashariki mwa Syria yasababisha vifo vya watu 23
China ni mojawapo ya nchi chache tu zilizo nje ya Mashariki ya Kati ambazo Assad amezitembelea tangu kuanza kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria mnamo mwaka 2011 ambavyo vimeua zaidi ya watu nusu milioni, kusababisha mamilioni ya wengine kuyahama makazi yao, na pia kuathiri miundombinu na viwanda vya Syria.
Ushawishi wa China unazidi kuongezeka katika eneo la Mashariki ya Kati
Ziara hiyo pia inakuja wakati ushawishi wa China unazidi kuongezeka katika eneo la Mashariki ya Kati.Mwaka huu China ilisimamia makubaliano ambayo yalishuhudia mahasimu wa muda mrefu wa kikanda Saudi Arabia na Iran inayoiunga mkono Syria zikikubaliana kurejesha uhusiano wa kidiplomasia na kufungua tena balozi zao katika mataifa hayo mawili.
Soma pia:Syria: Zaidi ya muongo mmoja wa mateso na mauaji
Hatua hiyo ilifuatiwa na kurejea kwa Syria katika kundi la mataifa ya Kiarabu wakati wa mkutano wa kilele ulioandaliwa nchini Saudi Arabia mnamo mwezi Mei na kutamatisha zaidi ya muongo mmoja wa kutengwa kikanda.