Rais wa Congo Felix Tshisekedi ziarani mjini Beni
17 Aprili 2019Ziara hii ikiwa ni ya kwanza katika eneo hili la Beni baada ya kuchaguliwa Desemba Mwaka jana, mamia kwa maelfu ya wakaazi wa Beni pamoja na Butembo walikwenda kwenye uwanja wa ndege wa Mavivi nje kidogo ya mji wa Beni, na wengine wengi wakimlaki rais katika barabara kuu ya mji huo.
Akiwahutubia wakaazi wa Beni kwenyi ofisi ya Meya wa Beni, rais Tshisekedi alizungumzia maswala ya amani katika eneo hili, hasa vita dhidi ya waasi kutoka Uganda ADF, pamoja na mapambano dhidi ya ugonjwa hatari wa Ebola.
Kuhusu vita dhidi ya waasi wa ADF, rais ameahidi kuwabadilisha wanajeshi ambao wameshapambana na kundi hilo la uasi kwa muda mrefu, na kuwaleta wanajeshi wengine pamoja na vifaa tosha.
Wakaazi wa Beni wahimizwa kufuata ushauri wa watalaamu juu ya Ebola
Kuhusu Ebola, rais huyo wa jamhuri ya kidemokrasi ya Congo, aliwashauri wakaazi wa eneo hilo kuheshimu ushauri unaotolewa na wataalamu juu ya namna ya kuudhibiti ugonjwa huo na kwamba hilo likifanyika huenda ugonjwa huo hatari ukatokomezwa kwa muda wa miezi mitatu.
Uitikiaji huo mkubwa wa wakaazi wa eneo hili kumlaki rais Tshisekedi, unafuatia mwito wa chama cha RCD/KML chake Antipas Mbusa Nyamwisi, ambae ni kiongozi wa kisiasa wa wakaazi wa eneo hili.
Wakati wa kampeni za uchaguzi wa Desemba 30 iliyopita, Nyamwisi alikuwa akimuunga mkono mgombea mwingine wa upinzani, Martin Fayulu. Uamuzi wake wa kuwahamasisha wakazi wa eneo hili kumpa mapokezi makubwa Rais Tshisekedi, umechukuliwa kama ishara kwamba Mbusa Nyamwisi sasa amesogea karibu na rais huyo mpya.
Nao wakaazi wa Beni waliomiminika kwa uwingi kuja kumlaki rais Félix Tshisekedi,waliiambia DW, kile wanachokisubiri kutoka kwake ni kuendeleza mbinu za kumaliza ugonjwa wa ebola na kutafuta amani ya kudumu ya eneo hilo.
Rais anakutana kwa mazungumzo leo Jumatano 17.04.2019 na wajumbe mbalimbali wa mashirika ya kiraia, wafanyabiashara, viongozi wa kiserikali pamoja na maofisa wa jeshi pamoja na polisi. Maswala ya amani,mpango wakukabiliana na ugonjwa wa Ebola, pamoja na usalama, ndio yatamulikwa katika mazunguzo baina ya rais na wajumbe hao.