1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Cuba Raul Castro akabiliwa changamoto za kuleta mabadiliko

Mwakideu, Alex25 Februari 2008

Rais mpya wa Cuba Raul Castro anakabiliwa na changamoto kubwa ya kujaribu kubadilisha maisha ya raia wa Cuba.

Raul Castro na nduguye Fidel Castro wakinong'onezana.Picha: AP


Rais mpya wa Cuba Raul Castro anakabiliwa na changamoto kubwa ya kujaribu kubadilisha maisha ya raia wa Cuba na kupatikana kwa vyakula nchini humo huku akitilia maanani kauli ya Ukomunisti iliyoanzishwa na nduguye Fidel Castro.


Wadadisi wa maswala ya kisiasa wanaamini kwamba Raul Castro aliechaguliwa na baraza la kitaifa hapo jana atafaulu kuleta mabadiliko machache ya kiuchumi katika nchi hiyo ambamo wananchi wanatatizika kupata chakula cha kila siku na mahitaji mengine ya kimsingi.


Raul mwenye miaka 76 alichukua uongozi wa Cuba tangu Julai mwaka wa 2006 pale aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Fidel Castro alipoanza kuugua. Punde tu baada ya kuchukua utawala wa nchi hiyo Raul aliahidi kuendeleza mabadiliko madogo madogo.


Lakini hata mabadiliko hayo madogo kama kuboresha utenda kazi wa serikali ya Cuba, kuongeza thamani ya pesa za Cuba na kupunguza kanuni za ukandamizaji yatachukua mda kukubalika katika siasa za Cuba.


Fidel Castro mwenye miaka 81 ambaye amekuwa mamlakani tangu aliponyakuwa mamlaka mwaka wa 1959 atabakia kiongozi anaetawala kichini chini licha ya kuondoka mamlakani wiki jana kwasababu za kiafya.


Raul Catro amesema uongozi wake hautatofautiana sana na uongozi wa kijamaa na kwamba ataendelea kuwasiliana na nduguye Fidel kuhusiana na maswala muhimu ya kitaifa.


Kiongozi huyo mpya amesema ataendelea kupigania mabadiliko na amemchagua mkomunisti Jose Ramon Machado Ventura kama Makamu wa Rais.


Maisha yanaendelea kama kawaida kwa wananchi milioni 11 wa Cuba ambao wengi wao walizaliwa chini ya utawala wa Fidel Castro baada ya waasi wake kuvamia kutoka katika milima ya Sierra Maestra na kuipindua serikali ya kidikteta iliyokuwa ikiongozwa na Fulgencio Batista aliekuwa akiungwa mkono na Marekani.


Wadadisi wanasema Raul Castro ataleta mabadiliko nchini Cuba lakini atakuwa akifanya hivyo kwa makini sana.


Wengi wao wanatarajia kwamba Raul ataondoa sheria kali zinazowakabili wafanyibiashara wadogo wadogo kama mafundi wa mitambo ya magari, wavuvi na wasanii wa kuchora na kuchonga vinyago.


Raul ambaye alikuwa mmoja wa viongozi wenye siasa kali alieogoza adhabu ya kifo kwa wapinzani wa mabadiliko amekuwa akihimiza mijadala katika miezi ya hivi karibuni na amekuwa akiwaomba raia wa Cuba waeleze hisia zao kuhusu maisha katika kisiwa hicho kilichoko karibean.


Raia wengi wamelalamika kuhusu maisha magumu yanayotokana na uchumi wa nchi hiyo ambao asilimia 90 yake unaendeshwa na serikali.


Carmelo Mesa Lago ambaye ni mzaliwa wa Havana na profesa katika chuo cha Pittsburgh anasema Raul ameinua matarajio ya wengi nchini Cuba kwa kugusia maswala ya mabadiliko na kuanzisha mijadala lakini iwapo ataleta mabadiliko machache tu ya kupumbaza wananchi basi atakua anaongeza mateso zaidi.


Raul anatarajiwa kuangazia maswala ya kimataifa kwa utaratibu licha ya Marekani ambayo imeiwekea Cuba vikwazo vya kiuchumi kwa miaka 46 kusema hapo jana kwamba inataka wafungwa wote wa kisiasa waachiliwe huru na uchaguzi wa vyama tofauti uitishwe ndio ibadilishe msimamo huo.


Raul Castro anaanza kazi hii leo kwa kumkaribisha Kadinali wa Vatican anaeshughulikia maswala ya nchi za nje Tarcisio Bertone, ambaye anatembelea Cuba akiwa na jukumu la kuongeza uhusiano wa nchi hiyo na kanisa katoliki.


Kanisa ndio eneo la kubwa la kipekee nchini Cuba lisiloongozwa na serikali na linatarajiwa kushiriki ipasavyo katika maswala ya kijamii wakati wowote wa mabadiliko ya uongozi.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW