Rais wa Ecuador asema wanajadili mustakabali wa Assange
27 Julai 2018Ecuador ilimpa hifadhi muanzilishi huyo wa mtando wa udukuzi wa WikiLeaks mwaka 2012, lakini anakabiliwa na kifungo nchini Uingereza kwa kukiuka masharti ya dhamana. Endapo ataondoka kwenye ubalozi huo, anaweza akashikiliwa na mamlaka za Uingereza na huenda pia akapelekwa nchini Marekani anakotakiwa na waendesha mashitaka kukabili tuhuma za kuvujisha nyaraka za siri za serikali.
Licha ya kukaa muda wote huo akiwa chini ya mikono ya Ecuador, leo Rais Lenin Moreno wa taifa hilo la Amerika ya Kusini amesema mjini Madrid, Uhispania, kwamba hakuna mtu anayepaswa kupewa hifadhi kwa muda mrefu.
Amesema mabadiliko yoyote ya hali ya Assage yanatakiwa yafanyike baada ya kuwepo majadiliano na pande zote.
Hata hivyo, Rais Moreno amesisitiza kuwa kuwa kuondolewa kwa Assange kunatakiwa kufanyike kwa njia iliyo sawa na inayofuata sheria:
Moreno ameongeza kuwa kile wanachokihitaji ni maisha ya mvujisha siri huyo anayesakwa nchini Marekani kutokuwa hatarini, lakini aliweka bayana kuwa haungi mkono ajenda ya kisiasa ya Assange akiwa kama mvujishaji wa nyaraka za siri, akisema kamwe hajawahi kuzipenda shughuli za mzawaliwa huyo wa Australia.
Mustakabali wa Julian Assange bado haujulikani
Bila shaka mazungumzo juu ya mustakabali wa Assange yanaendelea lakini hayakugusiwa wakati rais Rais Moreno alipokuwa Uingereza wakati wa ziara yake ya hivi karibuni alipohudhuria mkutano wa watu wenye ulemavu, alisema msemaji wa serikali ya Uingereza hii leo Ijumaa.
Wasiwasi juu ya mustakabali wa Assange umekuwa zaidi baada ya gazeti la Uingereza la Sunday Times kuripoti kuwa maafisa wa juu wa Ecuador na Uingereza wanajadili namna ya kumuondoa kutoka ubalozini baada ya ubatilishaji wa hifadhi yake. Mtu aliye karibu na mdukuzi huyo ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba hali ni mbaya zaidi.
Julian Assange mzaliwa wa Australia aliomba hifadhi katika ubalozi wa Equador mjini London ili kuzuia kupelekwa nchini Sweden kujibu maswali juu ya tuhuma za mashambulizi ya kingono anazoendelea kukanusha.
Anatakiwa pia nchini Marekani ambako anakabiliwa na tuhuma za kutoa siri za usalama wa taifa hilo kubwa duniani, ambazo kama akitiwa hatiani hukumu yake ni pamoja na kifungo cha maisha au cha muda mrefu jela.
Mwandishi: Amina Abubakar/Reuters/AP
Mhariri: Mohammed Khelef