Rais wa Ghana asisitiza uwekezaji zaidi barani Afrika
1 Machi 2018Amesisitiza kwamba mpango hivi sasa ni kuelekeza nguvu katika biashara na uwekezaji, kwa lengo la kuifanya Ghana kugharamia maendeleo yake yenyewe.
Uhusiano kati ya Ghana na Ujerumani hauko katika hali mbaya. Ghana inajikuta katika nafasi ya mfano kwa mataifa ya Afrika magharibi, amepigia upatu Kansela wa Ujerumani Angela Merkel . Viongozi hao wawili Merkel na Akufo Addo wanataka kuuimarisha zaidi ushirikiano uliopo katika suala la uchumi.
Ujerumani inafanya biashara na Ghana inayofikia kiwango cha euro milioni 584 kwa mwaka na kuifanya nchi hiyo kuwa mshirika muhimu wa Ujerumani katika bara la Afrika, licha ya kuwa ikilinganishwa na biashara na mataifa mengine duniani , Ghana iko nyuma sana. Akufo Addo alisema.
Uhusiano wetu na Ujerumani pamoja na mataifa mengine yanayoendelea unapaswa kulenga katika biashara na uwekezaji na sio katika kutoa misaada. Enzi za kutoa misaada ya maendeleo ilileta hali ya utegemezi , ambayo haikuweza kuisaidia Ghana hususan katika kufanya kazi kwa pamoja katika kile kinachojulikana kama mpango wa "Compact with Afrika" ikiwa na maana Pamoja na Afrika.
Mataifa hayo mawili yanataka kujenga dhana hiyo kwa pamoja. Juhudi hizo zinataka kuingizwa kwa uwekezaji zaidi wa makampuni binafsi katika Afrika. Ujerumani mwaka uliopita wakati ikiwa rais wa kundi la mataifa yaliyoendelea kiviwanda na yale yanayoendelea G20 ilianzisha juhudi hizo. Kansela wa Ujerumani amemwambia rais Akufo-Addo katika mazungumzo yao kwamba , "tunapaswa kuweka nguvu zetu zaidi ili uwekezaji wa makampuni binafsi kutoka Ujerumani kwenda Ghana ufanikiwe zaidi".
Mpango wa "Pamoja na Afrika"
Merkel amesema kwamba anatayarisha mkutano utakaofanyika hivi karibuni mjini Berlin, utakaozihusisha nchi wanachama wa mpango huo wa Compact ili kuangalia yale yaliyofikiwa.
"Waziri wa fedha wa Ghana anajishughulisha wakati huu na kufanikisha mpango huo wa Compact, kwa kufanya mabadiliko nchini Ghana. Na kwa upande wetu hapa Ujerumani tunataka kusaidia uwekezaji binafsi ambapo hadi sasa haujakuwa wa kutosha kwenda Ghana ili kuweza kutekeleza mpango huo".
Hadi sasa hata hivyo mpango huo wa "Pamoja na Afrika" kwa mtazamo wa kiuchumi haujaonesha mafanikio. Sera ya Ujerumani kuhusu Afrika inapaswa kuichukulia juhudi hii ya pamoja Afrika kwa undani zaidi, amedai mwenyekiti wa chama cha Afrika katika uchumi wa Ujerumani , Stefan Liebing, kabla ya mkutano baina ya Kansela Merkel na Akufo-Addo.
Wenye viwanda nchini Ujerumani, pamoja na halmashauri ya biashara ,wameikosoa serikali kwa kusema hadi sasa bado hakuna uhakika unaotolewa na serikali kwa wafanyabiasha wa Ujerumani, ambao wanataka kufanya biashara katika bara la Afrika.
Suala hilo liliwasilishwa kwa serikali katika miaka ya nyuma, suala ambalo kutokana na kampeni za uchaguzi na kipindi kirefu cha ujenzi wa serikali limewekwa kando. Hata serikali ya Ghana bado inakazi kubwa ya kufanya. Hususan kukatikati kwa umeme, lakini pia masuala ya ufisadi pamoja na hali mbaya ya elimu, hali inayowatisha wengi wa wawekezaji wa nje.
Katika mkutano wao Merkel na Akufo-Addo wamekubaliana kufanyakazi kwa pamoja katika kupambana na uhamiaji haramu. Vijana hawapaswi kupoteza nguvu zao katika jangwa la Sahara ama katika bahari ya Mediterania, badala yake watumie nguvu hizo kuijenga upya Ghana, amesema Akufo-Addo. Ujerumani inataka haraka warejeshwe nyumbani raia wa Ghana ambao waliomba hifadhi nchini Ujerumani na wakakataliwa. Kiasi ya Waghana 4,000 wanaishi hivi sasa nchini Ujerumani.
Mwandishi: Pelz, Daniel / ZR/ Sekione Kitojo
Mhariri : Caro Robi