Rais wa Guinea ya Ikweta, ajiandaa kubaki madarakani
21 Novemba 2022Rais huyo wa Guinea ya Ikweta Teodoro Obiang aliyemo madarakani kwa muda mrefu kuliko kiongozi mwengine yoyote barani Afrika amewania muhula mwingine. Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 80 ametawala kwa muda wa miaka 43 katika katika nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta.
Obiang aliingia madarakani mnamo mwaka 1979 baada ya kuuangusha utawala wa rais wa kwanza aliyeingia madarakani tangu nchi hiyo ilipopata uhuru wake kutoka kwa wakoloni wa Uhispania mnamo mwaka 1968. Katika uchaguzi uliofanyika hapo Jumapili Obiang anatarajiwa kupata zaidi ya asilimia 95 ya kura na hivyo kuendelea na muhula wa sita. Msimamizi wa vituo vya uchaguzi Maria Amparo Se Obama, ameeleza kuwa zoezi la upigaji kura lilikwenda salama.
Mchakato wa kuhesabu kura unaendelea na matokeo rasmi ya uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani yanatarajiwa kutangazwa katika siku chache zijazo. Wapinzani hawana matumiani ya kuambulia chochote katika uchaguzi huo na tayari wameeleza juu ya kutokea ubabaifu na mizengwe katika zoezi la kupiga kura. Andres Esono mmoja wa wagombea wawili wa pekee waliochuana na rais Obiang katika kinyang'anyiro cha urais amesema anachokifanya kiongozi huyo ni ulaghai mkubwa na mbaya zaidi kuliko wa hapo awali.
Soma Zaidi:Rais Nguema anayeiongoza Guinea ya Ikweta tangu 1979 atarajia kurudi tena madarakani
Esono amewaambia waandishi wa habari kuwa chama chake kimepokea malalamiko kutoka katika sehemu mbalimbali kwenye taifa hilo la Afrika ya Kati kwamba wapiga kura walilazimishwa kupiga kura zao hadharani badala ya kupiga kwa siri. Mgombea mwingine ni Buenaventura Monsuy Asumu, wa Chama cha Social Democrat Coalition,ambaye hapo awali alikuwa mshirika wa serikali.
Vyama 14 vya upinzani nchini humo vilijiunga kwenye muungano na chama tawala, ambacho mashirika ya kutetea haki za binadamu yanakilaumu kwa ukiukaji wa haki za binadamu, vitisho, kuwawinda wapinzani, utesaji, kupotezwa kwa watu na ufisadi. Serikali ya Obiang pia imelaumiwa kwa kuwaandama wanaodaiwa kupanga mapinduzi waliokimbilia katika nchi nyingine na kuwarudisha kwa nguvu nchini Guinea, ambapo walihukumiwa kifo.
Rais Obiang amesema ana matumaini ya chama chake cha PDGE kushinda tena katika uchaguzi huo mara baada ya kupiga kura pamoja na mkewe, Constancia Mangue de Obiang. Katika chaguzi zilizopita, Obiang hakuwahi kupata chini ya asilimia 90 ya kura ambapo mgombea Esono amesisitiza kwamba chama tawala kimefanya tena udanganyifu katika uchaguzi wa Jumapili.
Soma Zaidi:Guinea ya Ikweta yaandaa uchaguzi wa rais
Licha ya utajiri wake wa mafuta na gesi, taifa la Guinea ya Ikweta limo katika hali ya kushangaza ambapo pengo ni kubwa kati ya tabaka la watawala na idadi kubwa ya watu wanaoishi hasa kwa kutegemea kilimo cha kujikimu. Familia ya rais Obiang kwa muda mrefu inatuhumiwa kuishi katika utajiri mkubwa na kutumia fedha kutoka kwenye hazina ya serikali kufadhili mtindo wake wa maisha.
Mtoto wa rais Obiang, anayeitwa Teodoro Nguema Obiang Mangue, maarufu kama Teodorin, anatuhumiwa kwa ubadhirifu wa mali za serikali, huku baba yake akimpandisha cheo na kumtangaza kuwa makamu wa rais. Wadadisi wametabiri kwamba anaandaliwa kwa ajili ya kumrithi baba yake.
Mahakama ya Ufaransa mwaka jana ilimuhukumu Teodorin kwa makosa ya ufujaji wa pesa na ubadhirifu wa mamilioni ya fedha za umma. Alihukumiwa kifungo cha nje cha miaka mitatu na faini ya Euro milioni 30. Vilevile mahakama hiyo iliagiza kukamatwa mali zake za nchini Ufaransa zenye thamani ya mamilioni ya Euro.
Chanzo/AP