Rais wa Iran alisifu jeshi kulipiza kisasi kwa Israel
19 Aprili 2024Akiwahutubia mamia ya wananchi wa Iran katika mkoa wa Semnan siku ya Ijumaa (Aprili 19), kiongozi huyo hakugusia chochote kuhusu miripuko iliyotokea usiku karibu na mji wa Isfahan.
Kwa mujibu wa ripoti za shirika la habari la Tasnim, Mkuu wa Majeshi wa Iran Abdolrahim Mousavi amezungumzia tukio hilo la Isfahan kwa kusema mifumo ya ulinzi wa anga ilikidunguwa kifaa kinachotiliwa mashaka, na hakuna uharibifu uliotokea.
Soma zaidi: Hofu yaongezeka Mashariki ya Kati baada ya Israel kuishambulia Iran
Hata hivyo, mkuu huyo wa jeshi la Iran alisema uchunguzi ulikuwa unaendelea kutathmini ukubwa wa tukio hilo.
Kwa upande mwingine, msemaji wa idara inayohusika na masuala ya anga za mbali, Hossein Dalirian, alisema aina fulani ya droni iliyojaribu kuruka kwenye anga la Iran ilidunguliwa, lakini hakuna shambulio lolote la anga kutoka nje ya mipaka yake lililofanyika Isfahan au kwengineko katika nchi hiyo.