Rais wa Iran awaonya wanaoishambulia Yemen
5 Desemba 2017Mtoto wa rais wa zamani wa Yemen Ali Abdallah Saleh , aliyeuwawa na wanamgambo wa kihuthi , alitoa wito wa kulipiza kisasi dhidi ya makundi yanayoungwa mkono na Iran.
"Watu wa Yemen wanawafanya wachokozi wajutie hatua walizochukua," Rouhani amesema katika hotuba iliyotangazwa moa kwa moja katika televisheni. Matamshi yake yanakuja siku moja baada ya kuuwawa rais wa zamani Ali Abdallah Saleh na Wahuthi wanaoungwa mkono na Iran na kusababisha mashambulizi makali kutoka kwa majeshi yanayoungwa mkon na Saudi Arabia dhidi ya mji mkuu wa Yemen Sanaa.
Kamanda wa vikosi maalum vya jeshi la Iran, Mohammad Ali Jafari , amesema Saleh aliuwawa kwasababu alikuwa akijaribu kuuondoa uongozi wa Wahuthi kutoka madarakani.
Saleh hivi karibuni alivunja muungano wake wa mashaka uliodumu kwa muda wa mika mitatu na Wahuthi na kusema yuko tayari kwa mazungumzo na Saudia.
"Wasaliti Saudi Arabia wanataka kuleta hali ya wasi wasi wa kiusalama katika eneo hili chini ya amri kutoka Marekani wakifanyakazi kwa pamoja na Israel , tumeshuhudia juhudi zao za kuanzisha mapinduzi dhidi ya Wahuthi, ambayo yamekabwa mapema kabla ya kuzaliwa.
Ndege za majeshi ya muungano unaoongozwa na Saudi Arabia zimeshambulia maeneo ya mji mkuu yanayoshikiliwa na waasi alfajiri ya leo baada ya waasi kumuua rais wa zamani Ali Abdullah Saleh wakati akikimbia kutoka mji huo kufuatia kuvunjika kwa muungano wao , wakaazi wa mji huo wamesema.
Wito wa kupambana na Wahuthi
Rais anayeishi uhamishoni Abedrabbo Mansour Hadi ametoa wito kwa Wayemeni kujiunga pamoja dhidi ya wapiganaji wanaoungwa mkono na Iran. Karibu mashambulio saba yameangukia katika jengo la makao makuu ya rais katika eneo linaloishi watui wengi katikati ya mji wa Sanaa, wamesema watu walioshuhudia.
Kumekuwa na mapambano madogo madogo kati ya Wahuthi na waungaji mkono wa Saleh katika wilaya za kusini ambazo zimekuwa ni ngome kuu ya waungaji wake mkono.
Nae mtoto wa rais wa zamani Ali Abdullah Saleh aliyeuwawa ametoa wito wa kulipiza kisasa dhidi ya makundi yanayounga mkono Iran.
"Nitaongoza mapambano hadi Mhuthi wa mwisho atakapoondo9lewa kutoka Yemen, damu ya baba yangu itasikika katika masikio ya Iran, " alinukuliwa Ahmed Ali Saleh akisema. Amewataka waungaji mkono wa baba yake , "kuirejesha Yemen kutoka mikono ya wanamgambo wa Kihuthi wanaoungwa mkono na Iran".
Mkuu wa Umoja wa nchi ya Kiarabu Arab League Ahmed Abdul Gheit ameshutumu leo kuuwawa kwa rais wa zamani wa Yemen na waasi wa Kihuthi, akisema hali hiyo inaelezea juu ya hali msingi wa uhalifu wa kundi hilo. Mkuu huyo wa jumuiya ya mataifa ya Kiarabu ameonya kwamba kuuwawa kwa Saleh siku ya Jumatatu kunatishia kuripuka kwa hali mbaya ya usalama , katika nchi hiyo iliyoharibiwa kwa vita.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / afpe
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman