Rais wa Iran Pezeshkian aagiza kuanza mazungumzo na Marekani
2 Februari 2026
Kulingana na shirika la habari la Iran la Fars lililonukuu chanzo ambacho hakikutaka kutambulishwa, Rais Masoud Pezeshkian ameagiza kuanza kwa mazungumzo hayo na Marekani, ingawa hakikutaja tarehe hasa ya mazungumzo hayo.
Iran imesema mapema leo Jumatatu kwamba ilikuwa inafanyia kazi namna mazungumzo hayo yatakayofanyika na mpango mkakati utakaokuwa tayari katika siku zijazo, huku mataifa ya Ukanda wa Mashariki ya Kati huo yakichukua jukumu la kubadilisha mawasiliano kati ya pande hizo mbili.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Esmaeil Baqaei amewaambia waandishi wa habari kwamba tayari baadhi ya vipengele vimeshashughulikiwa na sasa wanachunguza na kumalizia maelezo ya kila hatua ya mchakato huo watakaoukamilisha siku zijazo.
Nchi za kikanda zaongeza juhudi za kutuliza mvutano
Amesema "Nchi za kikanda zina wasiwasi kuhusu hali ya sasa na zinajaribu kwa dhati kuchukua jukumu chanya, tofauti na nchi za Ulaya ambazo zinachangia kuongezeka kwa mivutano."
Baada ya mamlaka ya Iran kuchukua hatua kali dhidi ya waandamanaji mwezi uliopita, Rais Donald Trump wa Marekani alitishia kuivamia kijeshi na tayari ameagiza jeshi kupelekwa kwenye eneo la Mashariki ya Kati. Lakini katikati ya hatua hizo, Trump amesema ana imani ya kufikiwa kwa makubaliano na Tehran pia imesisitiza kwamba inataka diplomasia huku ikiahidi kujibu vikali uvamizi wowote.
Huku hayo yakiendelea, Waziri wa Mambo ya Nje Abbas Araghchi amezungumza kwa simu na wenzake wa Saudi Arabia, Misri na Uturuki kujadiliana kuhusu hatua za kikanda zilizofikiwa hadi sasa, hii ikiwa ni kulingana na shirika la habari la Iran, IRNA
Jordan: Hatutaruhusu anga letu kutumika kuishambulia Iran
Aidha, mwanadiplomasia mkuu wa Jordan Ayman Safadi amemwambia Araghchi kwamba hawataruhusu anga la taifa hilo kutumika kuanzisha mashambulizi dhidi ya Iran. Safadi ameongeza kuwa Amman aidha haitaruhusu upande wowote kukiuka anga lake ama kutishia usalama wake na wa raia wake.
Araghchi aidha anatarajiwa kukutana na mjumbe maalumu wa Marekani Steve Witkoff kuelekea mazungumzo hayo, limesema shirika la habari la Tasnim leo Jumatatu. Marekani lakini, haijathibitisha hilo. Marekani na Iran walifanya mazungumzo ya silaha za nyuklia mwaka uliopita, lakini walishindwa kuafikiana masuala kadhaa muhimu, na moja wapo likiwa ni shinikizo la Marekani la kuitaka Iran kusitisha kabisa programu yake ya kurutubisha madini ya urani.
Na huko jijini Paris, msemaji wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Anouar El Anouni amesema umoja huo unapinga uamuzi wa Iran wa kuyatambua majeshi ya nchi wanachama kama makundi ya kigaidi, baada ya wiki iliyopita Umoja huo kukiorodhesha Kikosi cha ulinzi wa Mapinduzi cha Iran kuwa kundi la kigaidi.
Tanbihi ya Mhariri: Makala hii awali ilijumuisha picha kutoka shirika la SalamPix. Iliondolewa tarehe 12 Machi 2026 baada ya Picture Alliance na Imago kutuarifu kuwa walikuwa wanaondoa picha za SalamPix kutokana na wasiwasi kuhusu chanzo chake na uwezekano wa kuwa zimehaririwa.