Rais wa Ivory Coast ametangaza kutowania muhula wa tatu
5 Machi 2020Rais wa Ivory Coast, Alassane Ouattara ambaye alizusha wasiwasi wa mda mrefu kuhusu hatma yake ya kisiasa ametangaza leo kwamba hatowania muhula wa tatu wa urais. ''Nawatangazia rasmi kwamba ninachukuwa hatua ya kutokuwa mgombea katika uchaguzi wa rais wa octoba 31, 2020 na kukabidhi madarakawa kizazi kipya''alisema Ouattara,mbele ya wabunge na maseneta waliokusanyika kwenye kikao maalumu mjini Yamoussoukro,mji mkuu wa nchi hiyo.
Kauli hiyo iliotolewa kufuatia hotuba yake ya dakika zaidi ya thelathini,ilipokelewa kwa makofi na vigelegele vya wabunge na wanafunzi wa shule za sekondari na chuo kikuu walioalikwa.
''Presi,Presi,Merci,Merci '' ( Rais rais ,asante, asante) walikuwa wakiimba wanafunzi hao.
''Tunafurahi sana na hatua yake ya kuwaachia madaraka vijana. Ni mtu anayeheshimu kauli yake. Ninafurahia sana kauli hiyo ya rais japokuwa mimi sio mfuasi wake''alisema Daouda bakayoko, mwanafunzi wa sekondari mjini yamoussoukro.
Ouattara, mwenye umri wa miaka 78 alichaguliwa kwa mihula miwili mwaka 2010 na 2015.Kukaribia kwa uchaguzi wa octoba kunazorotesha hali ya kisiasa nchini Ivory Coast ,miaka 10 baada ya vurugu za baada ya uchaguzi wa 2010 hadi 2011 ambazo zilisababisha vifo vya watu 3,000. Uchaguzi wa serikali za mitaa na madiwani wa 2018 uligubikwa na wizi wa kura na umwagikaji wa damu.
Marekebisho ya katiba
Kufikia sasa ni Guillaume Sorro aliekuwa spika wa bunge na kiongozi wa zamani wa waasi,ambae alijitangaza kuwa mgombea kwenye uchaguzi ujao.Marais wa zamani Henri Konan Bedie mwenye umri wa miaka 86 na Laurent Gbabo ambao ni wapinzani wa Ouattara hawajatangaza misimamo yao ikiwa watagombea au la.
Msimamo wa rais Alassane Ouattara umepongezwa na pande zote. Wengi wanaamini kwamba Ouattara atamuunga mkono waziri mkuu wake Amadou Gon Coulibaly kuwa mgombea wa urais,lakini wengi ndani ya chama chake wanahisi Coulibaly hana ushawishi mkubwa.
Kwenye hotuba yake rais Ouattara alipendekeza pia marekebisho ya katiba,huku akielezea kwamba marekebisho hayo hayawezi kumtenga mtu yeyote kuwania kwenye uchaguzi ujao. Kauli hiyo ni katika juhudi za kuwapa imani wapinzani ambao walielezea kwamba Ouattara anapanga njama ya kuwazuia baadhi ya wapinzani kutoshiriki kwenye uchaguzi wa octoba 31.
AFPE, Reuters