1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Kenya asema yuko tayari kuzungumza na Gen-Z

24 Juni 2024

Rais wa Kenya William Ruto amesema leo Jumapili kwamba yuko tayari kufanya mazungumzo na maelfu ya vijana waliofanya maandamano kwa amani wiki hii kote nchini kupinga mapendekezo ya nyongeza ya kodi.

Rais wa Kwnya  William Ruto
Rais wa Kenya William Samoei RutoPicha: DW

Maandamano hayo yaliandaliwa kwenye mitandao ya kijamii na kwa kushiriki maandamano hayo mabarabarani na vijana Wakenya wengi wenye umri mdogo maarufu kama ‘Gen-Z' ambao wamekuwa wakipeperusha maandamano hayo moja kwa moja kwenye mitandao ya kijamii.

Serikali ya Ruto imejikuta katika hali ya kuduwaa huku vijana hao wakiendelea kushinikiza kutoridhika kwao kuhusu sera za kiuchumi za serikai ya Rais Ruto.

Vijana waandamanaji katika mji wa Nakuru nchini Kenya wakipinga nyongeza ya kodiPicha: picture alliance / Sipa USA

Rais Ruto katika tamko lake la kwanza hadharani tangu kuanza maandamano hayo amesema "Ninajivunia sana vijana wetu, wamepiga hatua mbele kwa kufanya maandamano ya amani na ninataka kuwaambiakwamba tutawashirikisha,"

Ruto amesema serikali yake itafanya mazungumzo na vijana ili kwa pamoja walijenge taifa la Kenya liwe kubwa zaidi. Rais huyo wa Kenya ameyasema wakati wa ibada kwenye kanisa moja katika mji wa Nyahururu katika eneo la Bonde la Ufa nchini Kenya.

Gen-Z wenyewe wasemaje?

Hata hivyo bado upande wa waandaaji wa maandamano hayo ya kupinga ongezeko la kodi haujatoa majibu kama wanakubaliana na wito wa Rais Ruto au la lakini wameitisha maandamano mengine ya kitaifa mnamo Juni 25.

Licha ya Rais wa Kenya kuyaita maandamano hayo kuwa ni ya amani, wanaharakati wa haki za binadamu wameripoti vifo vya waandamanaji wawili kufuatia maandamano ya siku ya Alhamisi mjini Nairobi.

Soma Pia:Watu 200 wakamatwa maandamano ya ongezeko la kodi Kenya

Maandamano hayo kwa kiwango kikubwa yalikuwa ya amani, lakini maafisa walirusha mabomu ya kutoa machozi na maji ya kuwasha kwa siku nzima ili kuwatawanya waandamanaji waliokuwa karibu na Bunge.

Kulingana na taarifa ya maafisa wa Tume ya Haki za Binadamu ya Kenya, kijana Evans Kiratu mwenye umri wa miaka 21 alipigwa bomu la kutoa machozi wakati wa maandamano hayo na alifariki akiwa hospitalini.

Mnamo siku ya Ijumaa, polisi ya kenya ilisema inachunguza madai kukusu kupigwa risasi na maafisa wa polisi kijana mwenye umri wa miaka 29 jijini Nairobi baada ya maandamano hayo.

Soma Pia:Kijana wa pili athibitishwa kufa katika maandamano ya Kenya

Mamlaka Huru ya Kusimamia jeshi la polisi nchini Kenya Polisi (IPOA) imesema imeorodhesha kifo hicho kuwa ni matokeo ya mwanamume huyo kupigwa risasi na polisi mnamo siku ya Alhamisi.

Mashirika kadhaa, likiwemo la Amnesty International Kenya, yamesema takriban watu 200 walijeruhiwa katika maandamano hayo katika mji wa Nairobi, huku maelfu ya watu wakiingia barabarani kupinga mswada wa sheria ya kuongeza kodi kote nchini Kenya.

Serikali ya Rais William Ruto inayokabiliwa na uhaba wa fedha ilikubali kufanya mabadiliko baada ya mamia ya waandamanaji vijana kukabiliana na polisi katika mji mkuu wa Kenya.

Waandamanaji wapinga nyongeza ya kodi jijini Nairobi huku polisi wakitumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanyaPicha: LUIS TATO/AFP/Getty Images

Serikali ya Kenya yatetea nyongeza ya kodi

Utawala wa Ruto unatetea mipango ya kuongeza kodi kwa kiwango cha dola bilioni 2.7 ili kupunguza nakisi ya bajeti nchini humo. Inasema nyongeza za kodi zilizopendekezwa zinahitajika ili kuijaza hazina yake na pia ni hatua itakayoisaidia Kenya kupunguza utegemezi wa kukopa kutoka nje.

Kenya ina mlima wa deni, na gharama za kuyashughulikia ulipaji wa madeni zimeongezeka kutokana na kushuka kwa thamani ya sarafu ya nchi hiyo katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, hali inayoifanya serikali ya Rais Ruto kuwa kwenye kipindi kigumu.

Soma Pia:Wakenya waandamana kupinga ongezeko la kodi

Waandamanaji wanasema ongezeko la kodi mpya zinazopendekezwa katika muswada wa sheria ya fedha, zitaathiri uchumi na zitaongeza gharama za maisha kwa Wakenya ambao tayari wanakabiliwa na hali ngumu.

Kenya ni mojawapo ya nchi zenye uchumi unaonawiri katika eneo la Afrika Mashariki lakini thuluthi moja ya watu wake milioni 51.5 wanaishi katika umaskini.

Chanzo:AFP

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW