1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa zamani wa Korea Kusini Park Geun-hye apewa msamaha

24 Desemba 2021

Korea Kusini imesema itampa msamaha maalum Rais wa zamani wa nchi hiyo Park Geun-hye, ambaye alihukumiwa kifungo cha muda mrefu jela kutokana na mfululizo wa mashtaka ya rushwa yaliyomkabili.

Südkorea Park Geun-hye
Picha: Ahn Young-Joon/AP Photo/picture alliance

Wizara ya Sheria ya Korea Kusini imesema msamaha wa Park unalenga kukuza umoja wa kitaifa katika kukabiliana na matatizo yaliyosababishwa na janga la virusi vya corona. Rais huyo wa zamani anatarajiwa kuachiwa kabla ya mwaka huu kumalizika.

Park alikamatwa na kupelekwa gerezani mnamo mwaka 2017, baada ya kuondolewa madarakani kutokana na kashfa ya ufisadi hali iliyosababisha maandamano makubwa kwa miezi kadhaa. Miongoni mwa mashtaka makuu yaliyomkabili yalikuwa ni kula njama na rafiki yake wa muda mrefu, Choi Soon-sil, ambapo walishirikiana kuchukua rushwa ya mamilioni ya dola pamoja na kupokea fedha kutoka kwenye baadhi ya biashara kubwa nchini Korea Kusini ikiwa ni pamoja na kampuni ya Samsung.

Wafuasi wa aliyekuwa rais wa Korea Kusini Park Geun-hye Picha: Ahn Young-Joon/AP Photo/dpa/picture alliance

Mama huyo Park Geun-hye mwenye umri wa miaka 69 ni rais wa kwanza mwanamke aliyewahi kuchaguliwa nchini Korea Kusini. Alishinda uchaguzi uliofanyika  mwishoni mwa mwaka 2012 ambapo alimshinda rais wa sasa Moon Jae-in.

Aliungwa mkono na wahafidhina ambao walikuwa wafuasi wa baba yake aliyekuwa rais wa Korea Kusini waliyemuona kuwa ni shujaa aliyeinusuru nchi kutoka kwenye umaskini baada ya vita licha ya kukandamiza haki za kiraia kwa kiwango kikubwa.

Rais wa Korea Kusini Moon Jae-inPicha: Jeon Heon-Kyun/REUTERS

Ofisi ya rais Moon Jae-in imesema uamuzi wa kumsamehe Park unakusudiwa kuifuta historia mbaya ya zamani na badala yake kupalilia umoja wa watu wa Korea Kusini ili waungane mikono na kuwa kitu kimoja katika siku zijazo.

Rais Moon amesema anatumai kwamba hatua hii itatoa nafasi ya kuzika tofauti na kufungua enzi mpya ya ushirikiano na umoja, kwa mujibu wa msemaji wake. Msamaha maalum kama aliopewa Park Geun-hye unaweza tu kutolewa na rais nchini Korea Kusini. Uchaguzi ujao wa Korea Kusini unatarajiwa kufanyika mwezi Machi mwakani na wachambuzi wanasema hatua iliyochukuliwa na rais wa Korea Kusini ya kumsamehe Park Geun-hye itamuongezea sifa.

 

Vyanzo:/AFP/DPA/AP

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW