Rais wa Korea Kusini marufuku kuondoka nchini
9 Desemba 2024Amri hiyo imetolewa baada ya rais huyo kutangaza amri za kijeshi wiki iliyopita na kubatilisha baada ya muda mfupi.
Rais huyo pia alinusurika kura ya kutokuwa na imani naye bungeni.
Wakati huo huo, idara husika zinafanya uchunguzi juu ya amri ya kijeshi ya Rais Yoon iliyodumu kwa muda mfupi.
Mkuu wa idara ya uchunguzi ya nchini Korea Kusini amesema ametoa maagizo kwa maafisa wa idara hiyo kutaka bwana Yoon apigwe marufuku kuondoka nchini Korea kusini.
Hatua hiyo imethibitishwa na wizara ya mambo ya ndani.
Wakati huo huo, polisi nchini humo wamemkamata aliyekuwa waziri wa ulinzi, Kim Yong-hyun, wakati uchunguzi juu ya madai ya uhaini unafanyika.
Hatua ya kukamatwa kwa waziri huyo wa zamani inatokana na kuhusika kwake na sheria ya kijeshi iliyotangazwa na Rais Yoon Suk Yeol.
Ripoti za vyombo vya habari nchini humo zinaeleza kuwa waziri wa mambo ya ndani ambaye ni mshirika wa karibu wa Rais Yoon Suk Yeol, pia amejiuzulu.