Rais wa Korea Kusini Yoon akataa kuhojiwa na wapelelezi
16 Januari 2025Mahakama ya Kikatiba pia imeanza kikao cha pili cha kusikiliza kesi hiyo siku ya Alhamisi. Kesi hiyo itaamua kama iuidhinishe uamuzi wa bunge wa kumvua madaraka Yoon au la.
Yoon ndiye rais wa kwanza aliyeko madarakani nchini Korea Kusini kukamatwa na polisi. Rais huyo, ambaye anakabiliwa na mashitaka ya uasi, alihojiwa kwa saa nyingi jana lakini akatumia haki yake ya kikatiba kusalia kimya kabla ya kupelekwa katika jela ya mjini Seoul.
Wapelelezi kutoka Ofisi ya Uchunguzi wa Rushwa walitarajiwa kuendelea siku ya Alhamisi kumhoji Yoon, lakini timu yake imesema hatohudhuria. Wakili wake amesema rais huyo hatohudhuria kwa sababu za kiafya.
Yoon alisema alishirikiana na wapelelezi ili kuepusha umwagaji damu lakini hakubaliani na uhalali wa uchunguzi huo.
Wakati huo huo, maafisa wanajaribu kupata waranti mpya ambao unaweza kuruhusu ashikiliwe kwa zaidi ya saa 48.