Rais Yoon akabiliwa na jaribio jipya la kukamatwa
8 Januari 2025Rais wa Korea Kusini aliyesimamishwa kazi Yoon Suk Yeol anakabiliwa na jaribio jipya la kukamatwa baada ya mkuu wa timu ya uchunguzi kuapa kwamba watafanya kila liwezekanalo kuvunja vizuizi vyote vya ulinzi na kiusalama na kumchukua kiongozi huyo aliyefunguliwa mashtaka.
Mapema leo Jumatano waandamanaji wanaomuunga mkono na wanaompinga Yoonwalikusanyika karibu na makazi ya kiongozi huyo wakizozana baada ya mahakama kutoa waranti nyingine ya kumkamata kiongozi huyo ambaye aliiingiza nchi hiyo katika machafuko ya kisiasa mwezi uliopita kwa tamko la kuanzisha sheria ya kijeshi na tangu wakati huo amejificha katika makazi ya rais na kugoma kuitikia wito wa kwenda kuhojiwa na timu ya wachunguzi.
Oh Dong-woon, Mkuu wa Ofisi ya Uchunguzi wa kesi za Ufisadi kwa Viongozi wa Vyeo vya Juu (CIO) ambayo inaongoza uchunguzi huo dhidi ya Yoon ameomba radhi kwa kushindwa kwa jaribio la kukamatwa Yoon Ijumaa iliyopita baada ya mvutano mkali wa karibu saa sita katika makazi ya rais mjini Seoul.