Rais wa Lebanon azuru Qatar kuzungumzia mzozo wa Ghuba
29 Novemba 2021Kesho Jumanne rais Aoun atahudhuria ufunguzi wa michuano ya soka ya FIFA katika mataifa ya Kiarabu inayozikutanisha timu 16. Michuano hiyo ya siku 19 ni fursa kwa ulimwengu pia kuviona viwanja vipya vilivyojengwa Qatar, vitakavyotumika kwenye michuano ya kombe la dunia mwakani.
Mazungumzo ya ana kwa ana kati ya rais Michel Aoun na emir wa Qatar na maafisa wengine, yanafanyika wakati Lebanon ikizidi kuzama kwenye mzozo mbaya kabisa wa kiuchumi kuwahi kushuhudiwa katika zama hizi za sasa.
Kwenye mazungumzo hayo yanayofanyika Doha, Aoun atajadiliana kwa kina na viongozi hao masuala yanayohusu uhusiano kati ya Lebanon na mataifa ya Ghuba yanayoongozwa na Saudi Arabia. Rais Aoun ambaye ni mshirika wa kisiasa wa wanamgambo wa Kishia, amesema mara kwa mara kwamba Lebanon inataka uhusiano mzuri zaidi na Saudi Arabia.
Taifa hilo ambalo ni muungaji mkono wa jadi wa Lebanon, lilimuondoa balozi wake kutoka Beirut na mwezi uliopita iliuomba ujumbe wa Lebanon pia kuondoka nchini humo baada ya kuchukizwa na matamshi ya waziri wa habari wa Lebanon George Kordahi, aliyeviita vita vya Yemen ni `` upuuzi'' na uchokozi wa muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia.
Aoun asema ataisistiza Saudi Arabia kuwekeza nchini humo.
Muungano huo wa kijeshi ulijiingiza kwenye vitani, mwaka mmoja baada ya vita hivyo kuanza, ukitaka kuibakisha mamlakani serikali inayotambuliwa kimataifa na kuwafurusha waasi.
Aoun aliliambia gazeti la kila siku la Saudi Arabia la Al-Raya kwamba kwenye mazungumzo hayo, atamtolea mwito emir wa Saudia, Sheikh Tamin bin Hamad Al Thani kuwekeza kwenye ujenzi mpya wa bandari ya Beirutiliyoharibiwa vibaya na mlipuko mkubwa uliotokea mwaka jana. Amesema pamoja na ombi hilo, anakusudia kutafuta uwekezaji katika miradi ya miundombinu kama ya umeme, ambao hukatwa muda mwingi wa mchana.
Qatar yenye akiba kubwa ya gesi asilia ulimwenguni, huko nyuma ilikuwa mwekezaji mkuu nchini Lebanon.
Lakini Aoun ameenda Qatar, huku hali nchini mwake ikiwa si shwari kufuatia maandamano makubwa, na waandamanaji wakiweka vizuizi kwenye barabara zote kuu, wakielezea ghadhabu zao dhidi ya kundi la wanasiasa ambao kulingana na wao, ndilo lililosababisha mdororo wa uchumi na hali ngumu ya maisha.
Mataifa mengi yalikataa kuwekeza Lebanon ama kuisaidia serikali, hadi itakapotekeleza mageuzi ya kupambana na ufisadi na matumizi mabaya yaliyochochea anguko la uchumi mwaka 2019.
Soma Zaidi: Macron aionya Lebanon
Soma Zaidi: Macron kusimamia mkutano wa wafadhili kwa ajili ya Lebanon
Mashirika: APE