1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Liberia Weah akabiliwa na kura ngumu ya marudio

14 Novemba 2023

Rais wa Liberia George Weah, anakabiliwa na duru ya pili ya uchaguzi Jumanne akitafuta kumshinda mpinzani wake wa marudio na kupata muhula wa pili katika taifa hilo la Afrika Magharibi.

Liberia | Uchaguzi wa Rais.
Mwanamke akipiga kura yake katika duru ya pili ya uchaguzi wa Rais nchini Liberia mjini Monrovia, Jumanne, Novemba 14, 2023.Picha: Rami Malek/AP Photo/picture alliance

Nyota huyo wa zamani wa soka wa kimataifa huenda alimshinda kwa urahisi Joseph Boakai katika duru ya pili ya 2017, lakini matokeo ya duru ya kwanza ya kura mwezi uliopita yanaonyesha kukaribiana sana: Weah alipata asilimia 43.83 huku Boakai akijikinfia asilimia 43.44 ya kura jumla.

"Tunaenda kwenye uchaguzi ambapo hakuna mtu ana uwezo wa ushindani na tofauti kubwa," alisema Ibrahim Nyei, mkurugenzi mtendaji katika Taasisi ya Ducor ya Utafiti wa Kijamii na Kiuchumi.

Soma pia: Liberia yafanya uchaguzi wa rais na bunge

Katika wiki kadhaa tangu duru ya kwanza ya Oktoba 10, wagombea wote wawili wamekuwa wakitafuta ridhaa kutoka kwa vyama vingine vidogo vya upinzani. Kufikia sasa, Boakai amefanikiwa kuungwa mkono na washindi wa tatu, wa nne na wa tano.

Ingawa hiyo ni sawa na asilimia 5.6 tu ya kura, inaweza kuelekeza kura upande wa Boakai. Wakati huo huo, Weah amepata kuungwa mkono na vyama vingine viwili vya upinzani.

Rais wa Liberia George Weah.Picha: Peter Dejong/AP/picture alliance

Raia wa Liberia wanaweza kusubiri matokeo kwa muda mrefu: Iliwachukua maafisa wa uchaguzi wiki mbili kutangaza matokeo ya duru ya kwanza na haja ya kufanyika kwa duru ya marudio. Katika hotuba ya mwisho kwa wapiga kura, Weah alisisitiza kuwa "uchaguzi huu wa marudio sio tu wa kunichagua tena kama rais kwa muhula wa pili."

Soma pia: Waangalizi wa kimataifa waipongeza Liberia kwa uchaguzi wake

"Unahusu mustakabali wa Libeŕia. Unahusu watoto wenu, familia zenu, jumuiya zenu, na vizazi vijavyo,” Weah alisema. "Kwa pamoja, tutaendelea kutengeneza njia kuelekea maendeleo, amani na ustawi."

Ushindani mkali

Weah alishinda uchaguzi wa 2017 huku kukiwa na matumaini makubwa yaliyoletwa na ahadi yake ya kupambana na umaskini na kukuza maendeleo ya miundombinu. Ilikuwa ni mara ya kwanza kukabidhiana madaraka kwa njia ya kidemokrasia katika taifa hilo la Afrika Magharibi tangu kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya mfululizo kati ya 1989 na 2003 ambavyo viliua takriban watu 250,000.

Lakini rais huyo mwenye umri wa miaka 57 ameshutumiwa kwa kutotimiza ahadi muhimu za kampeni kwamba angepambana na ufisadi na kuhakikisha haki kwa wahanga wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.

Mgombea wa upinzani Joseph Boakai.Picha: Pulloh Moh-Marsi/Matrix Images/picture alliance

Boakai, 78, amefanya kampeni kwa ahadi ya kuinusuru Liberia kutokana na kile alichokiita uongozi uliofeli wa Weah. Hapo awali aliwahi kuwa makamu wa rais wa Liberia chini ya Ellen Johnson Sirleaf, kiongozi mwanamke wa kwanza barani Afrika kuchaguliwa kidemokrasia.

Soma pia: Marekani imetangaza vizuizi kwa watu wanaodhaniwa kudhoofisha demokrasi nchini Liberia

"Uchaguzi huu wa marudio unawakilisha msukumo wa mwisho wa kuondoa ugaidi, uvunjaji wa sheria, ufisadi, kutojali, kupuuzwa na uzembe ambao umeikumba nchi yetu kwa miaka sita," aliwaambia Waliberia katika hotuba yake ya mwisho kabla ya kura ya Jumanne. "Tuna imani kwamba Waliberia watajitokeza tena kwa wingi wao ili kuonyesha upendo wao, ujasiri, uthabiti, na azma ya kuungana nasi katika kuikomboa nchi yetu."

Chanzo: APE