1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMadagascar

Rais wa Madagascar aonya jaribio la mapinduzi jeshini

13 Oktoba 2025

Rais wa Madagascar Andry Rajoelina amesema jaribio la kuchukua madaraka kwa nguvu linaendelea, baada ya baadhi ya wanajeshi wa kikosi maalumu kujiunga na maandamano ya vijana wa Gen Z.

Madagascar Antananarivo 2025 | Wanajeshi waungana na maandamano dhidi ya Rais Andry Rajoelina
Askari wa kikosi cha jeshi la Madagascar wakisafiri kwa gari dogo la mizigo kuhakikisha usalama katika eneo la Ziwa Anosy, huku waandamanaji wakisherehekea kuwasili kwao baada ya mapigano kati ya waandamanaji na vikosi vya usalama wakati wa maandamano ya kudai kujiuzulu kwa Rais Andry Rajoelina mjini Antananarivo, Oktoba 11, 2025Picha: Luis Tato/AFP

Rais wa Madagascar Andry Rajoelina amesema jaribio la kuchukua madaraka kwa nguvu linaendelea nchini humo, baada ya baadhi ya wanajeshi wa kikosi maalum cha CAPSAT kujiunga na maandamano ya vijana wanaodai kujiuzulu kwake. Hata hivyo, hakukuwa na dalili za mapigano mitaani Jumapili, ingawa kulikuwa na uwepo mkubwa wa kijeshi katika mji mkuu, Antananarivo.

Kiongozi wa kikosi hicho, Kanali Michael Randrianirina, amekanusha madai ya mapinduzi lakini akasema wanajeshi wake "wametii wito wa wananchi.” Kikosi cha CAPSAT kimedai kuchukua udhibiti wa jeshi lote la Madagascar na kumteua Jenerali Demosthene Pikulas kama mkuu mpya wa majeshi.

Juhudi za Rais Andry Rajoelina kuwashawishi waandamanaji kumpa muda wa kufanya mageuzi wanayoyataka zimeshindikana na sasa jeshi linaonekana kumtupa mkono.Picha: Alexander Joe/AP Photo/picture alliance

Serikali ya Rajoelina imelaani vikali hatua hiyo, ikisema ni "jaribio la kuvuruga utulivu wa taifa” na kuwataka raia wote "kulinda katiba na uhuru wa taifa.” Haikujulikana mara moja rais yuko wapi, huku ripoti zikisema huenda amejificha kwa usalama wake.

Maandamano ya vijana wa "Gen Z Madagascar” yazidi kushika kasi

Kwa wiki tatu, taifa hilo la kisiwa chenye watu milioni 31 limekumbwa na maandamano makubwa zaidi tangu miaka mingi. Vuguvugu hilo la vijana wanaojiita "Gen Z Madagascar” lilianza kutokana na ukosefu wa maji na umeme lakini sasa limepanuka kudai mageuzi ya kisiasa na kujiuzulu kwa serikali.

Umoja wa Mataifa unasema watu 22 wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika maandamano hayo, ingawa serikali inapinga takwimu hizo. Kiongozi wa CAPSAT amesema askari wake walifyatuliana risasi na vikosi vya usalama vilivyokuwa vikijaribu kuvunja maandamano, na mwanajeshi mmoja wa kikosi hicho aliuawa.

Umoja wa Mataifa unasema takribani waandamanaji 22 wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa, lakini serikali inapinga takwimu hizo.Picha: Luis Tato/AFP/Getty Images

Madagascar ina historia ndefu ya migogoro ya kisiasa na mapinduzi ya kijeshi tangu ilipojipatia uhuru kutoka Ufaransa mwaka 1960. Rajoelina mwenye umri wa miaka 51 alichukua madaraka kwa mara ya kwanza mwaka 2009 baada ya mapinduzi yaliyoungwa mkono na jeshi, kisha akashinda uchaguzi wa mwaka 2018 na kurejea madarakani tena mwaka 2023.

Miito yatolewa kwa pande zote kuepusha vurugu

Maandamano ya sasa yameungwa mkono na vyama vya wafanyakazi na mashirika ya kiraia, yakilalamikia ufisadi, umaskini, gharama kubwa ya maisha na kukosekana kwa huduma bora za elimu na afya. Serikali imeweka amri ya kutotoka usiku katika mji mkuu na miji mingine mikubwa, huku waandamanaji wakiapa kuendelea hadi rais aondoke madarakani.

Marekani kupitia ubalozi wake Antananarivo imewaonya raia wake kubaki majumbani kutokana na hali "isiyotabirika na hatari.” Umoja wa Afrika nao umezitaka pande zote "za kiraia na kijeshi” kuepuka vurugu na kutumia njia za mazungumzo kurejesha utulivu.

Baada ya kusikiliza maamgizo kutoka juu kwa muda, baadhi ya vikosi vya Madagascar vimeamua kusimama na waandamanaji.Picha: Luis Tato/AFP/Getty Images

Rajoelina alijaribu kupunguza shinikizo kwa kuwafuta kazi mawaziri wote, akiwemo waziri mkuu, mwishoni mwa Septemba, lakini hatua hiyo haikutosha kuwanyamazisha waandamanaji. Vijana wa Gen Z, waliopata msukumo kutoka maandamano yaliyotikisa Nepal na Sri Lanka, wanasema "wanataka mabadiliko halisi, si maneno.”

Hali nchini Madagascar inabaki tete, huku jeshi likigawanyika na serikali ikijaribu kurejesha udhibiti. Dunia inasubiri kuona kama taifa hilo litarejea kwenye utulivu au kuingia tena katika mzunguko mwingine wa mapinduzi ya kijeshi.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW