1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ziarani Afrika

1 Juni 2009
Majaji katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ,The Hague.Picha: AP

Rais wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita leo ameanza ziara ya siku tano kulitembelea bara la Afrika kutafuta msaada kwa ajili ya mahakama, ambayo kwa kiasi kikubwa imepata sifa mbaya barani humo baada ya kumfungulia mashitaka Rais wa Sudan Omar Al Bashir.

Bw Sang Hyun Song ameanza ziara yake hiyo nchini Tanzania, ikiwa ni ya kwanza tangu kuwa kiongozi wa mahakama hiyo yenye makao yake mjini The Hague.

Ilikuwa ni mwezi Machi mwaka huu wakati Mahakama hiyo ya ICC ilipotoa hati ya kukamatwa kwa Rais huyo wa Sudan kwa tuhuma za uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu, katikia kipindi cha miaka sita ya mzozo wa Darfur, jimbo lililo magharibi mwa Sudan linalokabiliwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Rais Al-Bashir amekana shutuma zote hizo zinazomkabili.

Rais al Bashir anayetakiwa na mahakama hiyo .Picha: AP Photo

Katika taarifa yake aliyoitoa,kutangaza ziara yake hiyo, Rais wa Mahakama ya Kimataifa ya The Hague ameelezea umuhimu wa mahakama hiyo kufanya majadiliano na bara la Afrika ambalo limekuwa likiguswa sana na Mahakama hiyo toka kuanzishwa kwake.

Akiwa Tanzania Bw Song amekutana na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa nchi hiyo Bernard Membe na Waziri wa Sheria na Katiba wa nchi hiyo Mathias Chikawe.

Bwana Song pia ataitembelea Lesotho ambapo atafanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Bethuel Pakalitha Mosisili, pamoja na Botswana ambako atakua na mazungumzo na Rais wa nchi hiyo Ian Khama.

Aidha Rais huyo wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ataitembelea pia Afrika kusini, lakini kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ICC, akiwa huko hatokutana na viongozi wa serikali.

Pia hatokutana na Rais wa zamani Thabo Mbeki ambaye amepewa jukumu na umoja wa Afrika kumuakilishi rais al-Bashir katika suala hilo la mahakama hiyo ya kimataifa.

Mahakama ya uhalifu ya kimataifa inachunguza juu ya ukiukaji wa haki za binaadamu katika Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo na Jamhuri ya Afrika kati pamoja na Sudan. Bw Song ameseama atazishinikiza nchi za kiafrika zifanye marekebisho ya sheria zao zenyewe kuhusu uhalifu wa kivita, maovu dhidi ya binaadamu na mauaji ya kimbari ili isiwe lazima kesi za aina hiyo kusikilizwa tu mjini The Hague.

Mwandishi : Halima Nyanza /DPAE

Mhariri:M.Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW