Rais wa Mali ahimiza hatua za haraka
20 Oktoba 2012"Hatupaswi kupoteza hata sekunde moja. Hii ni dharura, hizi ni mbio dhidi ya wakati," Traore amesema katika hotuba kwa maafisa wa nchi za kigeni.
Washiriki wa mkutano huo baadaye walitoa taarifa ikisema kuwa mkutano huo umewapatia viongozi wa dunia, fursa ya kuungana katika mshikamano na watu wa Mali na kukubaliana , na serikali ya Mali, juu ya mpango wa kuchukua hatua , na kurejesha utaratibu wa katiba, umoja wa kitaifa na ardhi ya Mali.
Wameongeza kuwa mkutano huo, umeonesha ishara ya muungano wa Mali, katika diplomasia ya kimataifa.
Baraza la usalama
Mkutano huo umekuja wiki moja baada ya baraza la usalama la umoja wa mataifa kuidhinisha azimio linalotoa kwa mataifa ya Afrika magharibi siku 45 kupanga mikakati yao kwa ajili ya kuingilia kijeshi katika eneo la kaskazini la Mali.
Eneo hilo kubwa likiwa karibu sawa na nchi ya ufaransa liliangukia mikononi mwa makundi yenye itikadi kali ya dini ya Kiislamu katika mtafaruku ambao ulifuatia mapinduzi ya mwezi Machi mwaka huu nchini humo, nchi ambayo ilikuwa inatambuliwa kama yenye demokrasia imara kabisa katika bara la Afrika.
Wasi wasi kuwa eneo hilo linaweza kuwa maficho ya Waislamu wenye itikadi kali wa kundi la al-Qaeda kama ilivyokuwa Afghanistan muongo mmoja uliopita, majirani wa Mali pamoja na mataifa ya magharibi wana nia kuyaondoa makundi hayo yenye itikadi kali kutoka eneo hilo.
Katika miezi ambayo Waislamu hao wenye itikadi kali wamekuwa katika udhibiti wa eneo hilo, wameweka sheria zao kali za Kiislamu, Sharia, wakiwakamata wanawake ambao hawakujifunika , kuwapiga mawe hadi kufa watu wanaoishi pamoja bila ndoa na kuwakata viungo vya mwili watuhumiwa wa wizi, kwa mujibu wa wakaazi pamoja na makundi ya haki za binadamu.
Maeneo ya kale
Pia wameharibu maeneo ya kale yanayoheshimiwa na Waislamu, maeneo ambayo yamekuwa yakiheshimiwa kwa karne kadha na yamekuwa katika hadhi ya turathi za dunia, lakini Waislamu hao wenye itikadi kali wanayaona kama maeneo ya kukufuru.
Kiongozi wa Mali ameishukuru jumuiya ya kimataifa , na hususan umoja wa Afrika, umoja wa mataifa na mkoloni wa zamani Ufaransa, kwa kuiunga mkono nchini hiyo tangu kuzuka kwa mzozo huo.
Jumuiya ya uchumi ya mataifa ya Afrika magharibi ECOWAS imesema kuwa inaweza kutuma hadi wanajeshi 3,000 katika hatua ya kulikamata eneo la kaskazini.
Miongoni mwa viongozi waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na rais mpya wa halmashauri kuu ya umoja wa Afrika Nkosazana Dlamini - Zuma na rais Goodluck Jonathan wa Nigeria.
Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe
Mhariri : Bruce Amani