Rais wa Mali aivunjilia mbali kamati ya jeshi
3 Oktoba 2013Kuvunjiliwa huko kwa kamati inayowakilisha wanajeshi wa zamani inakuja kufuatia maandamano yaliyofanywa na wanajeshi wa ngazi ya chini mapema wiki hii katika kambi yao wakitaka kupandishwa madaraka waliyoahidiwa.
Wanajeshi hao walifyatua risasi hewani katika mji ulioko kusini wa Kati karibu na mji mkuu wa Mali,Bamako na kuwashika mateka wakuu wao.
Rais Keita alitangaza hapo jana kuwa ameagiza kuvunjiliwa mbali mara moja kwa kamati hiyo ya jeshi inayoongozwa na kiongozi wa zamani wa jeshi Kapteini Amadou Sanago kama mojawapo ya hatua za mchakato wa mageuzi katika vikosi vya usalama na ulinzi.
Utovu wa nidhamu hautavumiliwa Mali
Katika hotuba kwa nchi hilo la magharibi mwa Afrika linalojizoa zoa kutoka athari za mapinduzi ya kijeshi na misukosuko,Keita alisema hatavumilia utovu wa nidhamu na vurugu na kuongeza uchunguzi umeanzishwa kubaini sababu za maandamano hayo na waliohusika nayo.
Keita anayejulikana kwa jina maarufu nchini Mali kama IBK alikatiza ziara yake nchini Ufaransa na kurejea nyumbani ili kushughulikia uasi huo wa jeshi na kuzuka upya kwa mapigano kakskazini mwa nchi hiyo katika mji wa Kidal kati ya wanajeshi wa serikali na wapiganaji wa kundi la Tuareg.
Mapinduzi ya serikali mwezi machi mwaka jana yaliyochochewa na kushindwa kwa serikali kukabiliana na uasi wa kundi la waasi linalotaka kujitenga kwa eneo la kaskazini mwa nchi hiyo la Tuareg na kusababisha kukaliwa kwa eneo hilo na waasi wa kiislamu.
Mapigano yazuka upya Kidal
Jeshi la Ufaransa lilianzisha operesheni Mali mwezi Januari mwaka huu na kuwaua mamia ya wapiganaji wenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa al Qaeda na kuwafurusha kutoka eneo hilo la kaskazini lakini likawaacha waasi wa MNLA kusalia mjini Kidal likisema uasi wao ni suala la siasa za ndani ya Mali.
Ufaransa inatarajia kuwaondoa wanajeshi wake ifikapo mwishoni mwa mwaka huu lakini mapigano yamezuka upya kaskazini mwa Mali tangu MNLA kujiondoa kutoka mchakato wa kutafuta amani wiki iliyopita kwa shutuma kuwa serikali haiheshimu makubaliano yaliyoafikiwa.
Serikali kwa upande wake hapo jana iliwaachilia huru wafungwa 23 ambao ni waasi kuambatana na makubaliano ya Ougadogou ili kufufua mazungumzo na waasi.
Waziri wa sheria Ali Bathily amesema serikali inatumai kuachiliwa kwa wafungwa hao kutatuliza hali nchini humo na kurejesha amani.Serikali tayari imewaachilia wafungwa 32 chini ya mkataba wa amani uliotiwa saini katika nchi jirani ya Burkina Faso.
Mkuu wa kikosi cha kijeshi cha umoja wa Mataifa Mali Albert Koenders amezihimza pande zote mbili kurejea katika meza ya mazungumzo baada ya kuachiwa kwa wafungwa hao.
Mwandishi:Caro Robi /Reuters/dpa
Mhariri: Josephat Charo