Rais wa Mali kuunda serikali ya Umoja wa Kitaifa
28 Julai 2020Rais Ibrahim Boubacar Keita wa Mali ametangaza kuanzisha mchakato wa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa katika nchi hiyo inayoandamwa na machafuko baada ya kupata shinikizo kutoka viongozi wa mataifa ya Afrika Magharibi.
Rais Keita ameamua kuunda baraza la mawaziri wachache watakaopewa jukumu la kufanya majadiliano na upande wa upinzani kwa lengo la kuunda serikali ya pamoja.
Taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Mali imesema ili kukidhi matakwa ya jumuiya ya kikanda yaECOWAS, rais Keita ameamua kuunda baraza la mawaziri wachache watakao fanya majadiliano na upinzani.
Boubacar Salif Traoré, mtaalamu wa masuala ya kiusalama kwenye eneo la Sahel, amesema kwamba hatua hiyo ya Rais Keita haitoshi katika kutuliza hali ya kisiasa nchini Mali.
''Nafikiri tunaelekea kwenye hali ya kuweko na misimamo mikali baina ya pande hasimu.Kwa Na vitisho vya marais wa jumuiya ya ECOWAS vya kuwawekea vikwazo wale ambao watakao kiuka maazimio yao, havitachangia katika kuwapo na suluhisho la haraka.Waandamanaji bado wanashikilia msimamo wao wa kutaka rais ajiuzulu pamoja na serikali yake''.
Upinzani waapa kuandamana tena
Kwenye ujumbe huo wa mawaziri wachache walioteuliwa na rais Keita ni pamoja na waziri mkuu wa sasa; Boubou Cissé. Mawaziri watatu wamerejea katika nyadhifa zao za awali, ambao ni Waziri wa Ulinzi Ibrahima Dahirou Dembele, Waziri wa Utawala wa majimbo Boubacar Alpha Bah na Waziri wa Mambo ya Kigeni Tiebile Drame.
Wapya walioingia ni Kassoum Tapo aliyeteuliwa kuwa waziri wa sheria, Abdoulaye Daffe,mtu wa karibu wa mhubiri maarufu Mahmoud Dicko,kiongozi wa waandamanaji, aliyewekwa katika wizara ya fedha, na Bemba Moussa Keita ambaye amekabidhiwa wizara ya usalama wa ndani.
Waandamanaji wamekuwa mitaani kwa wiki kadhaa sasa kushinikiza kujiuzulu kwa rais Keita ambaye uongozi wake unaandamwa na kitisho cha makundi ya itakadi kali na uchumi unaodorora. Kwenye mkutano wa kilele kwa njia ya vidio hapo jana, viongozi wakuu wa nchi 15 za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Magharibi ya Afrika (ECOWAS) walisema wanamuunga mkono Rais Keita lakini wakatoa wito wa kuundwa serikali ya pamoja itakayojumuisha upande wa upinzani.
Jumuiya ya ECOWAS vile vile inalitaka bunge la Mali kujiuzulu ifikapo ijumaa ya Julai 31 na kuruhusu kuitishwa uchaguzi mpya.
Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lilitoa mwito kwa pande zote hasimu kutekeleza bila kuchelewa,maazimio ya mkutano wa marais wa jumuiya ya ECOWAS.Hata hivyo, waandamanaji wameahidi kurejelea maandamano tarehe 3 Agosti.