Rais wa Marekani Tump na Vyombo vya habari Magazetini
27 Februari 2017Tunaanzia Marekani ambako rais mpya Donald Trump anaonyesha kuzidisha makali ya msimamo wake dhidi ya vyombo vya habari. Anavunja miko , anasema hatoshiriki katika karamu ya chakula cha usiku pamoja na maripota wa ikulu ya White House. Gazeti la "Landeszeitung" linaendelea kuandika: "Ingekuwa Trump anakataa kushiriki katika karamu hiyo kwasababu hawezi kuvumilia lawama, pengine watu wasingeyakuza. Lakini Trump anaongoza kampeni dhidi ya waandishi habari asiowataka. Na mbinu zake za kutaka kuvinyamazisha vyombo vya habari, zitashindwa tu kwasababu sasa linazuka suala la sheria zinazodhaminiwa kikatiba. Na wamarekani wengi wanaitukuza katiba hiyo. Kinachotisha lakini ni kuona jinsi yeye, ambae ndie rais wa Marekani, anavyojaribu kuiendeya kinyume. Visa vyake vinalingana sana na vile vya watawala wanaotaka kugeuka waimla. Cha kutisha pia ni kwamba msimamo wa Trump unakorofisha juhudi za nchi za magharibi kukabiliana na nchi mfano wa Uturuki, Urusi au Ethiopia zinazowatia kishindo au kuwafumba midomo waandishi habari."
Kitisho cha siasa za kizalendo nchini Ufaransa
Kampeni za uchaguzi nchini Ufaransa zimepamba moto. Matokeo ya utafiti wa maoni ya wananchi yanaashiria vyama vikuu vya kisiasa vinakabiliwa na hatari ya kupigwa kumbo, uchaguzi wa rais utakapoitishwa miezi miwili kutoka sasa. Gazeti la "Mannheimer Morgen" linaandika: "Vyama vikuu vinatapatapa, vinahofia visije vikashindwa kuingia duru ya pili ya uchaguzi, kwasababu wao ndio wanaowakilisha "mfumo wa uongozi" ambao Marine Le Pen anataka kuung'owa. Chanzo cha kufanikiwa kwake kusonga mbele, kinaanzia katika hali duni iliyoko nchini humo hadi kufikia njia mbadala anayotaka kuifuata. Njia hiyo itakuwa na madhara makubwa sio tu kwa Ufaransa bali pia kwa Ulaya. Sasa jibu liwe la aina gani. Pengine jibu la maana lingekuwa kubuni utaratibu unaozingatia ukweli wa hali ya mambo : Ufaransa inahitaji mageuzi lakini sio yakujifungia na kufuata siasa za kizalendo. Ufaransa inastahili yaliyo mema zidi.
Waturuki kueneza kampeni za nyumbani Ujerumani
Mada yetu ya mwisho magazetini inahusiana na jinsi wanasiasa wa Uturuki wanaojaribu kueneza kampeni zao za uchaguzi hadi katika ardhi ya Ujerumani. Gazeti la "Lausitzer Rundschau" linaandika: "Mjadala kuhusu uwezekano wa rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan kuja Ujerumani kuwahutubia waturuki umepamba moto kutokana na kero kuwaona wahamiaji wakiihamishia katika ardhi ya Ujerumani mizozo iliyoko katika nchi zao za asili. Imeshawahi kushuhudiwa mizozo kati ya waisrael na wapalastina au ule kati ya Urusi na Ukraine na mingi mengine. Lakini waturuki wanaonyesha kwenda mbali zaidi na kufika hadi ya kukiuka sheria. Mfano pale Ozdemir alipozomewa na kutukanwa na dereva wa Taxi kwasababu ya kuunga mkono azimio linalowaunga mkono waarmenia. Hivi sasa hawezi kutoka bila ya mlinzi. Au pale maimam wanapofanya upelelezi dhidi ya waturuki wanaoishi humu nchini. Visa kama hivyo vinavyokwenda kinyume na sheria vinabidi viandamwe kikamilifu. Na hata dhidi ya wanadiplomasia wa Ankara, hatua zichukuliwe pindi wakenda kinyume na sheria.
Mwandishi:Hamidou Oumilkheir/INlandspresse
Mhariri:Yusuf Saumu