1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Mpito kuchaguliwa wakati ghasia zinaendelea CAR

20 Januari 2014

Rais mpya wa mpito anatarajiwa kuteuliwa leo katika jamhuri ya Afrika ya kati, wakati mawaziri wa Umoja wa Ulaya wanatarajiwa pia kuidhinisha jeshi litakaloingilia kati kutoa usaidizi kwa ujumbe wa kulinda amani.

Zentralafrikanische Republik Vereidigung Michel Djotodia
Rais wa mpito aliyejiuzulu Michel DjotodiaPicha: STR/AFP/Getty Images

Baraza la mpito la jamhuri ya Afrika ya kati linatarajiwa leo kumteua kiongozi mpya baada ya rais wa mpito Michel Djotodia pamoja na waziri wake mkuu wa mpito Nicolas Tiangaye kujiuzulu Januari 10 kutokana na mbinyo kutoka kwa viongozi wa kimkoa.

Djotodia na Tiangaye wameshindwa kuzuwia ghasia baina ya Wakristo na Waislamu ambapo mamia ya watu wameuwawa na wengine kwa mamilioni wamekimbia makaazi yao.

Michel DjotodiaPicha: Getty Images/Afp/Eric Feferberg

Wagombea

Wagombea wanane watawania nafasi hiyo , limesema bunge la nchi hiyo jana, huku kukiwa na ripoti za kuzuka tena kwa ghasia za kimadhehebu kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.

Shirika la kimataifa la msalaba mwekundu limesema jana kuwa kiasi ya watu 50 wameuwawa katika machafuko mapya yaliyozuka upande wa kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.

wanajeshi wa jeshi la kulinda amani la AfrikaPicha: P.Pabandji/AFP/GettyImages

Taarifa ya shirika hilo la msalaba mwekundu imesema , katika muda wa saa 48 zilizopita , vikosi vya shirika la kimataifa la msalaba mwekundu na chama cha msalaba mwekundu nchini humo vimezika miili ya watu 50.

Kanisa kimbilio la Waislamu

Katika mji wa Boali , kanisa la mji huo limekuwa sehemu ya kimbilio kwa Waislamu 700 wanaokimbia ghasia za kimadhehebu , ikiwa ni sehemu ya wimbi la nchi nzima la ghasia lililoanza kutokana na mapinduzi yaliyotokea Machi mwaka jana.

Hakuna mtu anayefahamu kwa uhakika nini kilichosababisha kuzuka kwa mapigano ya siku ya Ijumaa, lakini watu saba wanasemakana wameuwawa, Waislamu sita na Mkristo mmoja, na nyumba kadha zimeharibiwa.

Kiasi ya Waislamu 700 , wengi wao wanawake na watoto , wameishi kwa siku mbili sasa katika kanisa hilo, linalolindwa na wanajeshi 70 wa kikosi cha Ufaransa chenye jukumu la kurejesha utulivu katika nchi hiyo ya Afrika ya kati.

Wanajeshi wakilinda amaniPicha: P.Pabandji/AFP/GettyImages

Kwa ajili ya misa ya Jumapili , Waislamu walitoka katika kanisa hilo ili kuwapa nafasi waumini wafanye ibada.

"Tunapaswa kuacha kusababisha watu kupata mateso, amesema kasisi wa kanisa hilo katika ibada ya Jumapili , baadaye akiwataka waumini watoke nje na kuwasalimia majirani zao wa Kiislamu.

Baada ya misa Waislamu walirejea ndani ya kanisa hilo , wakiweka virago vyao sakafuni ama katika viti vya kanisa hilo.

Wanataka kuondoka

Baadhi ya Waislamu wamesema wanataka kuondoka kutoka nchi hiyo na kutafuta hifadhi nchini Cameroon nchi ambayo ina Wakristo wengi lakini pia idadi kubwa ya Waislamu. Tatizo ni usafiri. Waislamu hawawezi kusafiri bila ya kupewa msaada maalum na jeshi, kwa kuwa wanamgambo wa Kikristo wameweka vizuwizi barabarani karibu nchi nzima.

Rais wa mpito wa sasa Alexandre-Ferdinand NguendetPicha: Eric Feferberg/AFP/Getty Images

Wakati huo huo mawaziri wa mambo ya kigeni wa Umoja wa Ulaya wanatarajiwa leo kuidhinisha mpango wa Umoja huo wa jeshi litakaloingilia kati katika jamhuri ya Afrika ya kati, likitoa usaidizi kwa jeshi la Ufaransa na la Umoja wa Afrika ambayo tayari yako katika nchi hiyo.

Mkutano huo wa mawaziri mjini Brussels , utaangalia mipango ya kuingilia kati itakayodumu kwa muda wa miezi sita, ikilenga katika mji mkuu Bangui, ambako maelfu ya watu wamekimbilia katika makambi ya muda karibu na uwanja wa ndege, wakihitaji ulinzi kutoka katika jeshi la kimataifa.

Mwandishi : Sekione Kitojo / dpae / afpe

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW