Rais wa mpito wa Gabon amteua waziri mkuu mpya
8 Septemba 2023Kiongozi mpya wa kijeshi wa Gabon, Brice Oligui Nguema amemteua waziri mkuu mpya siku tatu baada ya kuapishwa kuwa rais wa mpito. Nafasi ya waziri mkuu itashikiliwa na Raymond Ndong Sima ambaye ni mkosoaji wa Ali Bongo Ondimba, aliyepinduliwa. Sima ambaye ni mchumi kitaaluma aliwahi kuwa sehemu ya serikali ya Bongo kuanzia mwaka 2012 hadi 2014, lakini alijiuzulu baada ya kutofautiana na rais na kujiunga na upinzani.Gabon yakubali mwongozo wa kurejea kwenye demokrasia
Nguema ambaye awali alikuwa mkuu wa kikosi cha walinzi wa rais aliahidi kuivusha nchi hiyo kuelekea katika mustakabali wa demokrasia imara baada ya mapinduzi. Muda mfupi kabla ya kupinduliwa kwake, Bongo alikuwa amechaguliwa kwa muhula wa tatu kwa mujibu wa matokeo rasmi, ingawa kulikuwa na mashaka ikiwa uchaguzi huo ulikuwa huru na wa haki.