1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Buhari ahimiza kusitishwa maandamano

23 Oktoba 2020

Buhari ameonya, serikali yake haitoruhusu mtu au kundi lolote kuvuruga amani ya taifa hilo, na kuwataka waandamanaji kupinga majaribu ya kutumiwa na waasi kuvuruga demokrasia changa ya taifa hilo.

Nigeria Abuja | Aussschreitungen
Picha: Kola Sulaimon/AFP/Getty Images

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari amelihutubia taifa Alhamisi usiku, kuhusu machafuko ambayo yameikumba nchi hiyo hivi karibuni, lakini la kushangaza zaidi katika hotuba yake rais hakutaja lolote kuhusu kupigwa risasi kwa waandamanaji wa amani katika eneo la Lekki Jumanne usiku.

Akizungumza kupitia njia ya televisheni Bukhari amesema kuwa serikali yake haitomvumilia mtu yeyote aliye na lengo la kudhoofisha usalama wa taifa na utulivu pamoja na kwenda kinyume na sheria.

Kulingana na Shirika la Amnesty Internatinal siku ya Jumanne usiku jeshi la polisi liliwafyatulia risasi waandamanaji waliokuwa wakiimba wimbo wa taifa na kusababisha vifo vya watu 12.

Mauwaji hayo yamelaaniwa vikali kutoka maeneo mbalimbali duniani lakini Buhari hakuzungumzia mauwaji hayo katika hotuba yake jana usiku badala yake aliwahimiza waandamanaji kusitisha maandamano.

Marekani imelaani machafuko hayo na kile ilichokiita utumiaji wa nguvu kupita kiasi wa jeshi la Nigeria kwa kuwafyatulia risasi waandamanaji wasio na silaha.

Vijana waaandamana dhidi ya ukatili wa polisiPicha: Benson Ibeabuchi/AFP

Buhari aidha amejibu ukosoaji ambao amepokea kutoka kwa wakuu wa nchi za Kiafrika na viongozi wengine wa ulimwengu na ametaka watafute ukweli wote unaopatikana kabla ya kuchukua msimamo, au kukimbilia kumuhukumu na kutoa matamko ya kumkejeli.

Buhari amesema "Kwa majirani zetu haswa na wanachama wa jamii ya kimataifa, ambao wengi wao wameelezea wasiwasi wao juu ya maendeleo yanayoendelea nchini Nigeria, tunawashukuru na tunawaomba nyote mtafute kujua ukweli wote unaopatikana kabla ya kuchukua msimamo au kukimbilia kuhukumu na kutoa matamko ya haraka."

Wakati rais Buhari anaendelea na hotuba yake Wanigeria walio na hasira walifurika katika mitandao ya kijamii kumshutumu rais.

Usman Okai Austin mmoja wa watumiaji ameandika "Rais Buhari wakati wa hotuba yake amekataa kutambua waliokufa kutokana na mashambulizi ya kijeshi kwa waandamanaji wa Lekki #EndSARS, "

"Kwa hotuba hii, inathibitishwa tuko peke yetu. Roho za kaka na dada zetu waliokufa katika # LekkiMassacre2020 na maeneo mengine kwenye maandamano ya #EndSARS pumzikeni  kwa amani. Inasikitisha, "aliandika Henry Okechukwu.

Machafuko ya ghasia yalizuka siku ya Jumatano huko Lagosna kusababisha uharibifu mkubwa na kuchoma vituo vya polisi, mahakama, vituo vya Televisheni na hoteli,  polisi walipambana kwa hasira na umati wa watu kwa kutumia vitoa machozi na risasi.

Katika sehemu nyingine za jiji lenye watu milioni 14 la Lagos, barabara na mitaa na maduka yalikuwa yamefungwa, baada ya amri ya kutotoka nje  kutolewa na serikali ili kuzuia machafuko. Waandamanaji wanaendelea kutumia mitandao ya kijamii kuendeleza hoja yao lakini wanapinga vikali vurugu hizo, ikisema maandamano yao yametekwa nyara na wahalifu

Moshi kutoka kwa gereza la Ikoyi mjini LagosPicha: Sophie Bouillon/AFP/Getty Images

Huku hayo yakijiri moshi ulionekana ukitoka katika kituo cha kurekebisha tabia cha Ikoyi na milio ya risasi kusikika, Tunde Oguntola, mkaazi wa karibu na gereza hilo amesema alisikia milio ya risasi kama askari na maafisa wa polisi walikabiliana na kile kilichoonekana kuwa jaribio  la wafungwa kutoroka gerezani.

Msemaji wa polisi Olamuyiwa Adejobi aliliambia Associated Press kwamba tukio ndani ya gereza "tukio lipo chini ya udhibiti, polisi wameingia kusaidia maafiisa wa gereza. " Hata hivyo hakuelezea hali halisi ndani ya gerza hilo.

"Maafisa wa polisi kwa sasa wanashika doria katika sehemu kuu za jiji kuhakikisha usalama wa wakaazi.Tafadhali kaeni ndani," amesema kamanda wa polisi jimbo la Lagos leo Ijumaa.

Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo ametaka uchunguzi kuanzishwa mara moja kuhusu vurugu na vikosi vya usalama, ambayo pia imesababisha Umoja wa Mataifa, Jumuiya ya Afrika, Jumuiya ya Ulaya kulaani matuo hayo.

 

AFP/dpa/AP/AFPE

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW