1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaNigeria

Rais wa Nigeria atangaza nyongeza ya muda ya mishahara

1 Oktoba 2023

Rais Bola Tinubu wa Nigeria amependekeza nyongeza ya muda ya mshahara kwa wafanyakazi wenye ujira mdogo pamoja na kupunguza gharama za usafiri wa umma katika juhudi mpya za kupunguza makali ya sera zake za uchumi.

Rais Bola Tinubu wa Nigeria
Rais Bola Tinubu wa Nigeria Picha: Gbemiga Olamikan/AP/dpa/picture alliance

Tangazo hilo amelitoa usiku wa kuamkia leo kupitia hotuba ya kuadhimisha miaka 63 ya uhuru wa Nigeria na ikiwa zimesalia siku mbili kabla ya vyama vikuu vya wafanyakazi kuitisha mgomo wa nchi nzima kupinga kupanda kwa gharama za maisha.

Amesema baada ya mazungumzo na vyama vya wafanyakazi na makapuni ya biashara, kima cha chini cha mshahara kwa wafanyakazi wa kipato cha chini kitapandishwa kwa dola 32 katika muda wa miezi sita ijayo.

Pia serikali yake inapanga kuharakisha uingizaji mabasi yanayotumia gesi kwa dhima ya kupunguza gharama za usafiri zilizopanda tangu serikali yake ilipoondoa ruzuku kwenye mafuta.

Rais Tinubu amewataka raia wa nchi hiyo kustahamili akisema mageuzi anayoyafanya ni magumu lakini yataleta neema siku zinazokuja.